Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amefanikisha kumaliza utata uliokuwa unakwamisha utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Mafinga unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 48.06.
Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi, salama, na ya uhakika kwa miji 28 nchini, ikiwemo Mafinga.
Katika ziara yake ya leo, Julai 25, 2025, Waziri Aweso amekutana na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Kikosi 841 Mafinga, Kanali Issa Daudi Chalamila, ambapo walikubaliana kumaliza ugumu uliokuwa umejitokeza kutokana na chanzo cha maji kilichozungukwa na eneo la jeshi.
Pia Waziri Aweso ametaka mkandarasi wa Kampuni ya Jundu Plumbers Ltd kuhakikisha kuwa wanakamilisha mradi kwa wakati, kwani Serikali tayari imeshalipa fedha zote zinazohitajika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amemuagiza Mkandarasi huyo kufanya kazi zote kwa wakati kabla mvua hazijaanza kunyesha.
Kukamilika kwa mradi huo kutaleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa Mafinga, ambapo takribani watu 95,505 watanufaika na huduma ya maji bora.
Aidha Huu ni mradi muhimu katika juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata huduma za maji bila vikwazo na kuondoa changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo mengi ya nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED