Waziri Aweso amkalia kooni mkandarasi Mradi wa Maji Wanging'ombe

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 05:55 PM Jul 22 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Wilaya ya Wanging’ombe na Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe, na kumuagiza mkandarasi Larsen & Toubro Limited kuongeza kasi ya utekelezaji kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wakati.

Waziri Aweso ametoa agizo hilo leo Julai 22, 2025, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 47.31. Aidha, katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 30 pekee, kinyume na lengo la kufikia angalau asilimia 80 katika kipindi hiki.

“Ninataka kuona kazi hii inafanyika kwa kasi. Hakuna sababu ya wananchi kuendelea kuteseka kwa kukosa maji wakati Serikali imeshatoa fedha na mkandarasi yupo kazini. Fanyeni kazi usiku na mchana,” amesisitiza Waziri Aweso.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo huo wa Miji 28 katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, ambapo alieleza kuwa kazi imefanyika kwa kiwango cha kuridhisha na matokeo yanaonekana.

1