MABILIONEA WANNE BARANI AFRIKA WENYE UTAJIRI WA WATU MIL 750

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 06:04 PM Jul 22 2025
Mabilionea wanne barani Afrika
Picha: Nipashe Digital
Mabilionea wanne barani Afrika

MABILIONEA wanne wa Kiafrika pekee, akiwamo Aliko Dangote, wana wastani wa utajiri wa dola bilioni 57.4 zaidi ya utajiri wa jumla wa Waafrika milioni 750 au nusu ya idadi ya watu wa bara hilo.

Hii huenda ikaonekana kuwa jambo la kushangaza, lakini ni ukweli uliofichuliwa na ripoti iliyochapishwa na shirika la Oxfam, Julai, 2025.

Mkusanyiko huu uliokithiri wa utajiri ni matokeo ya mtindo usio sawa wa kiuchumi unaopendelea matajiri zaidi, bila kujali huduma za umma na mapambano dhidi ya umaskini.

Oxfam inatoa wito wa kubuniwa kwa mfumo wa utozaji ushuru wa haki, ili kupunguza ukosefu wa usawa na ufadhili wa elimu, afya na maji ya kunywa.

"Sio kwamba Afrika haina utajiri; tatizo ni mfumo mbovu unaowawezesha watu wachache kujikusanyia mali nyingi huku wakiwanyima mamilioni ya watu huduma muhimu zaidi. Hii sio bahati mbaya. Ni kufeli kisiasa na mambo yanastahili kubadilika," amesema Fati N'Zi-Hassane, Mkurugenzi wa Afrika wa Oxfam.

Kulingana na Oxfam, mkusanyiko huu wa utajiri mikononi mwa watu wachache ni matokeo ya moja kwa moja ya mtindo usio na usawa wa kiuchumi, ambao huwanufaisha matajiri zaidi kutokana na mifumo ya kodi inayopendelea biashara na matajiri, misamaha ya kodi na ubinafsishaji wa sekta za kimkakati (kama vile nishati na mawasiliano), na wakati mwingine, mazoea ya biashara ambayo yanasisitiza wahusika wachache.

"Ukosefu wa usawa uliokithiri unatishia kudhoofisha demokrasia, kuzuia kupunguza umaskini na ukuaji, kuzidisha mgogoro wa hali ya hewa, kuzidisha dhuluma za kijinsia, na kusababisha kunyimwa haki za msingi na utu kwa raia wa kawaida," Oxfam inasisitiza.

Mabilionea hupata utajiri wao hasa kutokana na sekta kama vile madini, saruji, ujenzi na biashara ya kilimo viwanda vya hali ya juu na uwezo wa kifedha kujilimbikizia mali kwa urahisi.

Katika ripoti ya 2023 kuhusu ukosefu wa usawa, Oxfam ilihitimisha kuwa: "Kila bilionea anaashiria kufeli kwa mfumo wa kisiasa. Kadiri mabilionea wanavyoongezeka na kurekodi faida, wakati idadi kubwa ya watu wanakabiliwa na hali mbaya, umaskini unaoongezeka, na kupanda kway gharama ya maisha, ni ushahidi wa mfumo wa kiuchumi ambao unadhoofisha ubinadamu."

Ukosefu huu wa usawa umesababisha nchi nyingi kutoza ushuru kwa kuzikatia utajiri kamili badala ya mapato.

Kulingana na orodha iliyotolewa na jarida la Forbes mwanzoni mwa mwaka, mabilionea wanne bora wa Afrka ni Aliko Dangote wa Nigeria (saruji, sukari, mbolea, mafuta), Waafrika Kusini Johann Rupert (sekta ya bidhaa za anasa) na Nicky Oppenheimer (almasi), pamoja na Nassef Sawiris wa Misri (ujenzi na viwanda).

ALIKO DANGOTE DOLA BILIONI 23.3

Aliko Dangote ni mfanyabiashara wa Nigeria, aliyezaliwa Aprili 10, 1957, huko Kano, Nigeria. Anachukuliwa kuwa mmoja wa wajasiriamali wakubwa barani Afrika.

Mwanzilishi na mwenyekiti wa Dangote Group, kampuni kubwa ya viwanda, mara kwa mara anaorodheshwa kama mtu tajiri zaidi barani.

Aliko Dangote ni jina tajika katika sekta kadhaa za biashara: saruji, sukari, chumvi, unga, pasta, mbolea, mafuta na gesi.

Familia yake tayari ilikuwa inajihusisha na biashara ya kilimo nje ya nchi lakini, Dangote aliweza kubadilisha urithi huu kwa kujenga himaya ya viwanda.

Mnamo 1977, akiwa na umri wa miaka 20, baada ya kupata mkopo kutoka kwa mjomba wake, Dangote alianzisha biashara ndogo ya kuuza vyakula mjini Lagos. Aliagiza mchele, sukari na saruji kutoka nje ya nchi, kuuza nchini Nigeria.

Baada ya kubainisha kuwa biashara ya uagizaji kutoka nje pekee ukuaji wake ni mdogo, Kkatika miaka ya 1990 na 2000, Dangote aliamua, kuwekeza katika uzalishaji wa ndani ili kudhibiti faida kwa:

Ujenzi wa viwanda vya sukari na chumvi; Uundaji wa mitambo ya kusaga unga. Uzinduzi wa kampuni ya Dangote Cement, na kuwa mzalishaji mkubwa wa saruji barani Afrika

Mkakati huu wa uzalishaji wa ndani badala ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi ulimuwezesha kupunguza gharama, kuongeza viwango vyake na kutawala soko.

Tangu miaka ya 2010, Dangote imepanua shughuli zake katika sekta mpya za kimkakati: ujenzi wa mojawapo ya viwanda vikubwa zaidi vya kusafisha mafuta duniani, vilivyozinduliwa mwaka 2023, uzalishaji wa mbolea na uwekezaji katika kilimo na usafiri.

Baadaye akaanzisha Kmpuni ya Dangote Group nje ya Nigeria, kujenga viwanda vya saruji katika mataifa ya Senegal, Ethiopia, Tanzania, Afrika Kusini, n.k., akiimarisha nafasi yake mjasiriamali wa Afrika nzima.

JOHANN RUPERT DOLA BILIONI 14.2 

Johann Rupert alirithi biashara ya familia kutoka kwa baba yake, Anton Rupert na kuikuza hadi kuwa kampuni ya thamani ya mabilioni ya dola ya bidhaa za kifahari.

Rupert ni mfanyabiashara wa Afrika Kusini, aliyezaliwa tarehe 1 Juni 1950 huko Stellenbosch, Afrika Kusini. Anajulikana sana kwa kuwa mkuu wa Richemont Group, mojawapo ya makampuni makubwa ya kifahari duniani.

Rupert ni mwana wa Anton Rupert, mfanyabiashara wa viwanda wa Afrika Kusini ambaye alianzisha Rembrandt Group (baadaye Remgro), kampuni ambayo hapo awali ililenga tumbaku kabla ya kujiingiza katika biashara mbalimbali.

Johann Rupert alirithi sehemu ya utajiri huu kutokana na jukumu lake wakati wa mabadiliko na upanuzi wa kampuni.

Mnamo 1988, Johann Rupert alianzisha kampuni ya Richemont nchini Uswizi, kwa msingi wa mali ya kimataifa ya Rembrandt.

Richemont inafahamika kwa mtengenezaji wa bidhaa za kifahari, mmiliki wa chapa mashuhuri kama vile Cartier, Van Cleef & Arpels, Montblanc, Piaget, IWC na Vacheron Constantin.

Kampuni hiyo kwanza iliangazia saa, vito na vifaa vya kifahari, sekta inayopitia ukuaji mkubwa wa kimataifa.

Kulingana na Forbes (2025), Johann Rupert mara kwa mara anaorodheshwa kama mmoja wa wanaume tajiri zaidi barani Afrika, na utajiri unaokadiriwa wa karibu dola bilioni 15.

Wakati mwingine amemzidi Aliko Dangote katika nafasi ya juu ya Afrika kulingana na mabadiliko ya soko la hisa.

NICKY OPPENHEIMER DOLA BILIONI 10.2 

Nicky Oppenheimer ni mtu wa pili tajiri zaidi nchini Afrika Kusini. Nicky, aliyezaliwa Juni 8, 1945, ni bilionea wa Afrika Kusini na mmoja wa watu mashuhuri katika tasnia ya almasi.

Yeye ni mrithi wa kizazi cha tatu wa familia ya Oppenheimer, ambayo ilijengwa kimsingi kupitia udhibiti wao wa De Beers, moja ya kampuni kuu za almasi ulimwenguni, na Anglo American, kampuni ya kimataifa ya uchimbaji madini.

Nicky Oppenheimer alisoma katika Shule ya Harrow nchini Uingereza na kisha Christ Church, Oxford, ambako alihitimu na shahada ya Siasa, Falsafa na Uchumi.

Mwishoni mwa miaka ya 1970, Nicky alijiunga na biashara ya familia na kupanda ngazi, hatimaye kuwa Makamu wa Rais wa Anglo American na kisha Mwenyekiti wa De Beers.

Chini ya uongozi wake, De Beers alibadilika kutoka kampuni inayolenga sekta ya madini na kuwa biashara mseto zaidi, kutilia mkazo zaidi katika uwekaji chapa na uuzaji wa reja reja.

Mwaka wa 2012, alifanya uamuzi wa kihistoria wa kuuza hisa 40 za familia yake katika De Beers kwa kampuni ya Anglo American kata takriban dola bilioni 5.1, kuashiria mwisho wa udhibiti wa karne ya Oppenheimer wa himaya ya almasi.

Japo alistaafu kutoka kwa De Beers, Bw. Oppenheimer anasalia kuwa mtu mashuhuri katika ulimwengu wa biashara. Tangu wakati huo amejikita katika kusimamia utajiri wa familia yake kupitia kampuni ya kibinafsi ya uwekezaji ya Stockdale Street na amejikita katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kilimo, uhifadhi, na mtaji wa ubia.

Pia anajihusisha sana na juhudi za uhisani, hasa katika nyanja za elimu, uhifadhi, na uchumi wa kijamii.

NASSEF SAWIRIS DOLA BILIONI 9.4 

Kufikia mwanzoni mwa 2025, bilionea huyo wa Misri alikuwa na takriban dola milioni 264, baada ya kurekodi ongezeko la dola milioni 310 mnamo 2024.

Nassef aliyezaliwa Januari 19, 1961, ni mfanyabiashara bilionea wa Misri na mmoja wa watu tajiri zaidi barani Afrika na katika ulimwengu wa Kiarabu.

Ni mtoto wa mwisho wa Onsi Sawiris, mwanzilishi wa muungano wa Orascom.

Nassef Sawiris ambaye amesomea masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, anatokea katika familia ya Sawiris iliyo na ushawishi, mojawapo ya nasaba kubwa zaidi za biashara nchini Misri.

Anaorodheshwa mara kwa mara kama mtu tajiri zaidi nchini Misri na mmoja wa tajiri zaidi barani Afrika na ulimwengu wa Kiarabu.

Mnamo 2023, OCI iliunganisha kampuni zake za mbolea katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini za ADNOC na kuunda ADNOC Fertiglobe, huku OCI ikisalia kuwa mbia mkubwa zaidi.

Yeye ndiye mwanahisa mkubwa zaidi wa kampuni kubwa ya michezo ya Ujerumani adidas AG, ambapo anamiliki takribani 10% mapato yake kupitia kampuni yake ya uwekezaji ya NNS Holding BV. Dau hili linajumuisha sehemu kubwa ya utajiri wake.

Utajiri wake unabadilika kulingana na soko na bei za bidhaa, lakini kwa ujumla inakadiriwa kuwa na kati ya dola za Marekani bilioni 8 na 9 (kuanzia katikati ya 2024/2025).

Vyanzo vyake vikuu vya utajiri ni hisa zake katika kampuni za OCI/ADNOC Fertiglobe, Adidas na Lafarge Holcim.

Nassef Sawiris ni mfadhili mkuu katika Wakfu wa Sawiris anayojishughulisha na masuala ya maendeleo ya kijamii, iliyoanzishwa na baba yao. Taasisi hiyo inasaidia miradi ya elimu, afya na maendeleo ya kiuchumi nchini Misri.

Yeye binafsi alitoa dola milioni 20 kwa Chuo Kikuu cha Chicago (ambacho alihitimu) kuchangia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Misri.

Chanzo: BBC