Maofisa wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza wamefariki dunia baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kuhama njia na kupinduka kufuatia dereva kuchoka na kusinzia akiendesha maofisa hao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Safia Jongo imetaja maofisa hao kuwa ni Emmanuel Leonard (33) pamoja na Mwita John (28) wote Maofisa Forodha na wakazi wa Buswelu wilayani Ilemela.
Jongo amesema ajali hiyo ilitokea Julai 20, 2025 majira ya saa kumi usiku katika eneo la Bwawani-Katoro barabara ya Katoro-Chibingo wilayani Geita.
Amesema ajali hiyo ilihusisha gari la serikali aina ya Toyota Land Cruiser, lenye namba za usajili STM 3696, mali ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza.
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari hilo Julius Dismas (31) Mkazi wa Mwananchi Mwanza kupatwa na uchovu na kushindwa kulimudu gari.
“Uchunguzi umebaini kuwa dereva Dismas alipatwa na uchovu uliomsababisha kushindwa kumudu gari. Kutokana na hali hiyo gari lilihama upande wake wa barabara ,” amesema Kamanda Jongo.
Aidha amesema dereva huyo alipozinduka usingizini na kujaribu kulirejesha gari upande wake kwa haraka, lilipoteza mwelekeo na hatimiye kupinduka na kusababisha vifo na uharibifu wa gari.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa madereva wote kuhakikisha wanazingatia viwango vya usalama barabarani na kuwa waangalifu na kupumzika vya kutosha kabla au wakati wa safari ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika,” amesema Kamanda Jongo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED