WATANZANIA wamehimizwa kutumia vyema sanaa na teknolojia zilizopo katika kuhamasisha wanawake na vijana, kushiriki kwenye nafasi mbalimbali za uongozi kisiasa na kiuchumi na kuleta maendeleo ya kweli kuelekea uchaguzi mkuu, Oktoba, mwaka huu.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, amesema hayo leo, wakati akifungua mdahalo wa siku moja kwa viongozi 30 kutoka sekta mbalimbali za kisiasa, biashara, dini, vyombo vya habari, sanaa na utamaduni kutoka mikoa ya Rukwa, Katavi, Dodoma, Morogoro Dar es salaam na Pwani.
Mdahalo huo umeoandaliwa na taasisi za YOGE na ONA Stories na kufanyika mjini hapa.
Kilakala amesema mashirika yasiyo ya kiserikali kwa sasa yanaonekana yakichagiza uhuru wa kuwapa nafasi za uongozi kwa wanawake na vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi, kwa lengo la kuleta mabadiliko.
Amesema kama Taifa wamepiga hatua kubwa katika masuala ya usawa wa kijisnia, ushiriki wa wanawake na vijana kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ukilinganisha na kipindi kilichokuwa cha upiganiaji wa uhuru wa Tanganyika.
Mkurugenzi wa shirika la Usawa wa Kijinsia, Haki, Mazingira na Vijana (YOGE), Philomena Mwalongo, amesema washiriki wamefanikiwa kutazama filamu ya kumbukizi ya maisha ya Bibi Titi Mohamed, mtetezi na kiongozi mwanamke, aliyetoa mchango mkubwa katika kuhimiza ushiriki wa wanawake na vijana katika uongozi na nafasi za maamuzi nchini.
Amesema filamu hiyo imelenga kuonesha mchango wake chanya na katika kuchochea na kuhakikisha ushiriki endelevu wa wanawake na vijana kwenye nafasi za juu za uamuzi nchini.
Ofisa Utamaduni Manispaa ya Morogoro, Safia Kingwahi, amesema malengo ya mdahalo huo, ni kuwakumbusha harakati za kupigania uhuru zilizofanywa na Bibi Titi, unaokumbusha wananchi uzalendo, kupata ari ya kupigania nchi, bila kujali kama ni mwanamke au mwenye ulemavu wowote ule.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED