Barabara ya vumbi Hospital ya Rufaa Shinyanga kujengwa lami

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 11:36 AM Jul 22 2025
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu akimkabidhi Mkandarasi Hati ya ujenzi wa Barabara ya Lami Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kutoka Nguzonane hadi Mwawaza.
Picha: Marco Maduhu
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na watu wenye ulemavu akimkabidhi Mkandarasi Hati ya ujenzi wa Barabara ya Lami Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kutoka Nguzonane hadi Mwawaza.

Mbunge wa Shinyanga Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, amemkabidhi mkandarasi eneo la kuanza rasmi ujenzi wa Barabara ya Lami ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutoka Nguzonane hadi Mwawaza, pamoja na ujenzi wa Stendi mpya ya Mabasi Kizumbi.

Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika maeneo ya miradi hiyo na kushuhudiwa na viongozi wa Serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM), watendaji wa halmashauri pamoja na wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katambi alisema kilio cha wananchi wa Shinyanga juu ya ujenzi wa barabara ya kuelekea Hospitali ya Rufaa kwa kiwango cha lami kimesikilizwa, na hatua ya mkandarasi kukabidhiwa eneo ni ushahidi wa Serikali kusikia na kutenda.


“Natoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu hii ili idumu kwa muda mrefu, maana tumehangaika sana kuhakikisha fedha za ujenzi zinapatikana,” alisema Katambi.


Kuhusu ujenzi wa stendi mpya ya mabasi, Katambi alieleza kuwa mradi huo utachochea mzunguko wa fedha katika mkoa huo, kutoa ajira kwa vijana na kuinua uchumi wa wananchi wa Shinyanga.

“Tunataka takribani Shilingi bilioni 26 zinazotekeleza miradi hii zibaki hapa Shinyanga. Hii ni kwa kuhakikisha ajira zinatolewa kwa wakazi wa eneo husika, na vifaa vya ujenzi vinanunuliwa kutoka kwa wafanyabiashara wa hapa,” alisisitiza.


Alitoa maelekezo kwa mkandarasi kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ubora wa hali ya juu, kwa kuzingatia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati, kama mkataba unavyoelekeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anord Makombe, alisema amefarijika kuona hatua ya ujenzi inaanza rasmi, hasa kwa kuwa barabara ya kwenda hospitali ya rufaa ilikuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi.

Awali, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Alexius Kagunze, alisoma taarifa ya miradi hiyo, ambapo alieleza kuwa Serikali imepata ufadhili kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya kilomita 4.6 kutoka Nguzonane hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, pamoja na barabara nyingine ya kilomita 1.6 kutoka Senatoni kupitia Ndala hadi kuungana na barabara ya hospitali hiyo.


“Gharama za jumla za miradi hii ni Shilingi bilioni 26, na utekelezaji wake utachukua miezi 15, huku muda wa matarajio ukiwa miezi 12. Mkataba ulisainiwa Juni 26, 2025 jijini Dodoma,” alieleza Kagunze.


Mkandarasi anayeitekeleza miradi hiyo ni Kampuni ya SIHOTECH, ambapo Harson Mchau, ambaye ni msimamizi wa miradi, aliahidi kutekeleza kwa ubora wa hali ya juu na kukamilisha kwa wakati.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo, akiwemo Shida Juma, walieleza kufurahishwa kwao na kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo muhimu, wakisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na changamoto za vumbi na mashimo, hasa kwa wagonjwa wanaoelekea Hospitali ya Rufaa.