Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), mkoani Mara, imeunda kamati itakayokuwa na kazi ya kupambana na upotevu wa maji ambao umekuwa ukitokea.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe wa kutoka ofisi ya Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na Ofisi ya Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Wajumbe wengine ni kutoka Ofisi ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bunda (OCD), ofisi za mkuu wa huduma za serikali wilaya ya Bunda, ofisi ya Katibu Tawala Wilaya ya Bunda na baadhi ya Wataalamu kutoka BUWASSA ambao ndio mwenyeji wa kamati hiyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASSA, Esther Gilyoma wakati akitambulisha kamati kwa watumishi wa mamlaka hiyo na kufafanua kuwa itasaidia kukomesha.
Amesema mbali na kuunda kamati hiyo, mamlaka yake iko mbioni kufunga mita za maji ambazo kila mteja atatumia huduma ya maji kulingana na kiasi cha fedha atakachokuwa analipa.
"Tumepata mita zaidi ya 1,000 zitakazomwezesha mteja kulipia huduma za maji kabla ya kutumia na kupunguza malalamiko ya kulipia bili za maji ni kama LUKU za umeme," amesema Esther.
Amesema mita hizo zitatumika katika maeneo yote yenye mtandao wa maji wa BUWASSA, na kwamba upatikanaji wa maji Bunda umefikia asilimia 85, huku mamlaka hiyo ikiwa na wateja zaidi ya 10,000.
Mita mpya zina faida nyingi, ikiwamo kupunguza malalamiko ya wateja kulimbikiziwa bili, kumwezesha mteja kupanga matumizi ya maji kulingana na kipato chake, kumwondolea mwenye nyumba kero ya kulipa bili iliyotumiwa na wapangaji baada ya wao kuondoka," amesema.
"Kwa muda mrefu BUWASSA imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu bili za maji, sasa imepata mwarubaini utakaomaliza kero hiyo kwa kuwawezesha kulipia maji kabla ya kuyatumia kulingana na uwezo wao," amesema.
Kuhusu upotevu wa maji, Mhandisi wa mamalaka hiyo, Vumilia Alex amesema asilimia 31.2 ya maji hupotea kila mwezi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo baadhi ya watu wasio waaminifu kuyaiba na kufanyia shughuli zao bila kusomeka kwenye mita.
"Watu wanafunga mipira nyuma ya mita kitendo ambacho haiwezi kusoma na kutumia kumwagilia bustani, kufyatulia matofali au wenye hoteli kujali katika visima vikubwa," amesema Mhandisi Vumilia.
Mhandisi Vumilia amesema kuwapo kwa kamati ya kupambana na upotevu wa maji pamoja na mita mpya, vitasaidia kumaliza tatizo hilo la muda mreji katika mjini wa Bunda na vitongoji vyake.
"Kwa kuwa mkurugenzi ameunda kamati na pia kuna LUKU, kama ilivyo katika umeme ambapo wateja hununua token kuchaji ili kupata huduma ya nishati, kwenye maji sasa utaratibu ni huo, hivyo ninaamini tunakwenda kuondokana na malalamiko na upotevu wa maji," amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED