Mamia ya wanafunzi wanaotaka kusoma kozi mbalimbali nje ya nchi wamejitokeza kwenye maonyesho ya vyuo vikuu nje ya nchi ambapo wengi wamepata udahili wa papo kwa papo.
Maonyesho hayo yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam na kushirikisha vyuo zaidi ya 20 kutoka nchi mbalimbali yanatarajia kufanyika tena kwenye mikoa ya Dodoma na Arusha hivi karibuni.
Hayo yalisemwa leo kwenye maonyesho hayo jijini Dar es salam na Mkurugenzi wa wakala wa Elimu Nje ya nchi, Global Education Link, Abdulmalik Mollel.
“Tulitarajia tuanze saa nne asubuhi lakini tulipofika tu saa moja tukakuta utitiri wa wanafunzi hata kabla hatujafungua kwa hiyo kwa kweli mwitikio umekuwa mkubwa sana wanafunzi wamekuja kwa wingi sana na wengi wamepata udahili,” amesema
Mollel amewataka watanzania wanaotaka kusomea nje ya nchi kuchangamkia ufadhili unaotolewa na vyuo mbalimbali ambavyo vinatoa ufadhili kwa asilimia miamoja.
Amesema kwenye maonyesho hayo na ambayo yanakwenda kufanyika mikoa mingine kama Arusha na Dodoma wanafunzi wanaotaka kusomea baadhi ya kozi wanaweza kupata ufadhili wa kuanzia asilimia 20 hadi asilimia 100 ya masomo.
“Kwenye maonyesho haya yanayofanyika Dar es Salam kuna vyuo vitatu vya nje ya nchi ambavyo vinatoa ufadhili kwa asilimia 100 kwa watu wanaotaka kusomea Shahada za Uzamili na Uzamivu yaani PhD kwa hiyo sisi Global tunaona hii ni fursa nzuri sana kwa watanzania,” amesema
Amesema maonyesho hayo pia yamekuwa yakitumika kutoa ushauri kwa wanafunzi wanaotaka kwenda kusoma vyuo vya nje kuhusu kozi ambazo wanataka kwenda kusoma kwani wengi wamekuwa wakishindwa kufahamu vyema vyuo vinavyotoa kozi wanazopendelea.
“Imekuwa kawaida wanafunzi kukosa nafasi kwenye vyuo vya hapa ndani kutokana na uchache wa nafasi kwani mahitaji ni makubwa sasa kwenye maonyesho haya kuna vyuo kama 20 unachagua chuo na unakotaka kwenda kusoma mapema,” amesema Mollel
Amesema mwitikio umekuwa mkubwa kwa wanafunzi wanaotaka kwenda kusoma nje ya nchi ambao wameshiriki kwenye maonyesho hayo na kupata udahili.
Amesema vyuo vilivyoshiriki kwenye maonyesho hayo vimepata ithibati kwenye nchi zao na vinatambuliwa na Tumeya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hivyo wanafunzi wanaopata fursa wanakuwa na uhakika wa kusoma vyuovinavyotambulika.
Amesema vyuo hivyo vimebobea kwenye masuala ya teknolojia na uhandisi na vimekuwa na mchango mkubwa wa kuzalisha wataalamu kwenye nchi wanakotoka hali ambayo imesababisha uchumi wa nchi hizo kuwa mkubwa.
Mollel amesema baada ya maonyesho ya Dar es Salaam watakafanya maonyesho kama hayo mkoani Arusha na kisha watafanya mkoani Dodoma wakiwa na vyuo vikuu nje ya nchi kwaajili ya kudahili wanafunzi.
“Tumejitahidi kuwaletea vyuo vikuu bora sana kwasababu tunataka Tanzania ipate wataalamu waliobobea kwenye nyanja mbalimbali. Na kozi zote ambazo vyuo vikuu nje ya nchi vimekuja nazo ni za kimkakati kama uchumi wa buluu, afya, uhandisi na uhandisi katika kompyuta ambapo tunatarajia watapatikana wataalamu wa akili mnemba ambayo mahitaji yake ni makubwa,” amesema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED