Hatifungani ya TANGA UWASA yaanza kuzaa matunda

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:23 AM Jul 22 2025
Hatifungani ya TANGA UWASA yaanza kuzaa matunda.
Picha; Mpigapicha Wetu
Hatifungani ya TANGA UWASA yaanza kuzaa matunda.

Hatimaye wakazi wa mikoa ya Tanga, Pangani, Muheza na Mkinga wananufaika moja kwa moja na matunda ya hati fungani ya kijani iliyotolewa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Jijini Tanga (TANGA UWASA), yenye thamani ya Shilingi Bilioni 53.12, ambayo ilianza kuuzwa rasmi tarehe 22 Februari 2024.

Katika hatua kubwa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, amekabidhi vifaa mbalimbali vya ujenzi wa miundombinu ya maji, ikiwemo mabomba na viunganishi vyake, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 6.3. Vifaa hivyo vitatumika kupanua wigo wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya mradi.

Kwa mujibu wa Dk. Batilda, utekelezaji wa mradi huo unalenga kufanikisha upatikanaji wa maji safi kwa asilimia 100 katika Jiji la Tanga, asilimia 95 kwa Wilaya ya Pangani, na huduma ya maji kwa saa 24 kwa wakazi wa Mkinga.

“Leo hii ni siku muhimu tunapopokea mabomba haya na viunganishi vyake. Niwatake wakandarasi wote wanaoshiriki katika mradi huu kuhakikisha wanatekeleza kwa ufanisi na kukamilisha kwa wakati ili wananchi wanufaike kama ilivyokusudiwa,” amesisitiza Dk. Batilda.

Aidha, ameeleza kuwa mafanikio ya mradi huu ni zao la ubunifu wa TANGA UWASA katika kutumia hati fungani ya kijani kama njia mbadala ya kupata fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za maji.

“Huu ulikuwa ubunifu mkubwa. Leo hii tunaona matokeo chanya ambayo yanagusa maisha ya mtu mmoja mmoja. Ni lazima tuendelee kudhibiti maeneo yote yenye uvujaji wa maji ili kupunguza upotevu,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANGA UWASA, Mhandisi Geofrey Hilly, amesema kuwa mradi wa hatifungani ya kijani unahusisha ujenzi wa mtandao wa mabomba yenye jumla ya urefu wa kilomita 170, ambapo sehemu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 55 tayari imekabidhiwa.

“Mradi huu unalenga kuboresha huduma ya maji katika wilaya nne: Tanga Jiji, Muheza, Pangani na Mkinga. Unapokamilika, takribani wakazi 555,000 watanufaika. Wale ambao hawajafikiwa na huduma watafikiwa, na maeneo yenye miundombinu chakavu yataboreshwa,” amesema Mhandisi Hilly.

Ameongeza kuwa mradi huo pia unahusisha upanuzi wa vyanzo vya maji kutoka uwezo wa lita milioni 42 hadi milioni 72 kwa siku, na upanuzi wa mtambo wa kusafisha maji kutoka lita milioni 45 hadi milioni 60 kwa siku. Hii itaongeza uhakika wa upatikanaji wa maji katika wilaya zote zilizopo katika mradi.

1
zan
2