Wawili wakamatwa kwa kuzuia askari kufanya kazi yao

By Remmy Moka , Nipashe
Published at 07:04 PM Jul 22 2025
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa

Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu wawili, James Kululema (42) na Aisam Oscar, kwa tuhuma za kuendesha gari katika hali ya ulevi, kufanya fujo, na kuzuia askari kutekeleza majukumu yao ya kisheria.

Akizungumza na vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa, amesema tukio hilo lilitokea katika barabara ya Kamanga-Sengerema baada ya askari wa usalama barabarani kupata taarifa kuhusu gari lililokuwa limeegeshwa katikati ya barabara na kuzuia watumiaji wengine.

“Askari walipofika eneo hilo walimkamata dereva James Kululema, mkazi wa Tambuka Reli mkoani Geita, aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T.226 DPV aina ya Subaru Forester kwa kosa la kuegesha gari katikati ya barabara,” alisema Mutafungwa.

Ameongeza kuwa wakati askari wakiendelea na mahojiano, alijitokeza Aisam Oscar ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kapripoint wilayani Nyamagana, akiwa ameshika chupa za pombe na kuwafanyia askari fujo kwa kujaribu kumzuia dereva huyo kuhojiwa.

Watuhumiwa wote wawili kwa sasa wanaendelea kuhojiwa kwa makosa mbalimbali. James Kululema anashikiliwa kwa tuhuma za kuendesha gari akiwa amelewa, kuegesha gari kimakosa, na kuzuia askari kutekeleza wajibu wao.

Aidha, Aisam Oscar anahojiwa kwa kosa la kuruhusu gari lake kuendeshwa bila bima halali pamoja na kosa la kuingilia kazi za askari polisi.

Kamanda Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi linaendelea na doria za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza kuhakikisha usalama wa barabarani unaimarishwa, na kwamba mara baada ya uchaguzi, watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yao.