Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, zimebakiza siku moja kutamatishwa, huku Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan akiweka rekodi ya mikutano yake kufuatiliwa na asilimia 90 ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, mikutano ya kampeni ya mgombea urais wa chama hicho, imefuatiliwa na watu milioni 57.1 kupitia vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii.
Idadi hiyo ni sawa na takriban asilimia 90 ya Watanzania wote kwa mujibu wa makadirio ya idadi ya watu yam waka 2024 yaliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), iliyoonyesha Tanzania ina watu milioni 63.6.
Kwa maneno mengine, katika kila watu 10 nchini, tisa wamefuatilia mikutano ya kampeni za Dkt Samia, ama kupitia vyombo vya habari au kupitia mitandao ya kijamii.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo, Jumatatu Oktoba 27, 2025 jijini Mwanza, Kihongosi amesema mbali na waliofuatilia kwa njia hiyo, watu milioni 25.3 walihudhuria mikutano hiyo moja kwa moja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED