Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kumfyatulia risasi na kumsababisha kifo mwananchi aitwaye Frank Sanga, Julai 19, 2025, wakati wakiwa katika doria ya pikipiki katika eneo la Ntyuka, jijini Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Agathon Hyrera, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Julai 21, 2025, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini humo.
Kamanda Hyrera amesema tukio hilo lilitokea majira ya saa 8:00 mchana katika Kata ya Ntyuka, ambapo askari hao walimkamata marehemu Frank Sanga akiwa anaendesha pikipiki bila leseni wala kuvaa kofia ya usalama, huku akiwa amebeba magunia matatu ya mkaa.
"Baada ya kukamatwa, askari walimuelekeza waende wote kituoni ili makosa yake yashughulikiwe kisheria. Hata hivyo, alikataa na kudai hawezi kwenda mpaka ndugu zake wafike," amesema Kamanda Hyrera.
Baada ya muda mfupi, ndugu zake walifika wakiwa kwenye pikipiki tatu zenye abiria zaidi ya wawili kila moja, na kuanza kuwalazimisha askari hao waachilie pikipiki ya marehemu na wamkabidhi funguo ili waendelee na safari yao.
Kamanda Hyrera amefafanua kuwa hali hiyo ilisababisha mvutano, ambapo baadhi ya ndugu hao walianza kuwashambulia askari. "Askari mmoja alifyatua risasi hewani kujaribu kuwatawanya, lakini mmoja wa ndugu aliendelea kumshambulia askari kwa fimbo hata baada ya askari huyo kuanguka chini," alieleza.
Katika mazingira hayo ya hatari, askari huyo alifyatua risasi nyingine na kumpiga Sanga sehemu ya paja na nyonga. Marehemu alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, lakini alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini.
Jeshi la Polisi limeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na kuwashikilia askari waliokuwa kwenye doria hiyo kwa ajili ya hatua zaidi.
"Uchunguzi unaendelea kwa kuhoji pande zote ili kubaini kwa undani mazingira ya tukio. Kama itabainika kuwa askari alitumia nguvu kupita kiasi, hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa," amesisitiza Kamanda Hyrera.
Aidha, Kamanda huyo ametoa wito kwa wananchi kuepuka tabia ya kujichukulia sheria mkononi au kujaribu kupokonya silaha kutoka kwa askari.
"Jeshi la Polisi limepewa mamlaka ya kubeba silaha kwa ajili ya kulinda amani na usalama wa wananchi. Hata hivyo, silaha hiyo hutumika pia kumlinda askari anayeibeba. Wananchi wanapaswa kushirikiana na askari badala ya kuanzisha vurugu," ameongeza.
Kwa sasa, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya taratibu nyingine za uchunguzi na mazishi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED