Kiwango cha VVU Geita chapungua

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 03:12 PM Jul 21 2025
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela ametaja kuwapo na mafanikio mbalimbali katika sekta ya afya mkoani humo ikiwamo kupungua kwa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kutoka asilimia 5.1 mwaka 2021 hadi kufikia 4.90 mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma katika Mpango wa Idara ya Habari Maelezo wa kueleza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita, Shigela amesema katika sekta hiyo kumekuwapo na kuimarika kwa miundombinu ya kutolea huduma za afya, kuongezeka kwa upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi ambayo imechangia mafanikio ya sekta hiyo. 

Ametaja baadhi ya miundombinu ya sekta hiyo iliyojengwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni Hospitali za Halmashauri za Bukombe, Chato, Geita, Geita Manispaa, Mbogwe na Nyang’hwale, idadi ya zahanati kutoka 129 mwaka 2021 hadi 198 mwaka 2025 na vituo vya afya kutoka 25 mwaka 2021 hadi 42 mwaka 2025.