KLABU ya Singida Black Stars, imedaiwa kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji, Idrissa Diomande, kutoka Zoman FC ya Ivory Coast, huku ikimtema winga wake aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu uliopita, Victorien Adebayor.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimesema kuwa timu hiyo imekamilisha dili hilo kwa lengo la kukiimarisha kikosi ambacho msimu ujao kitashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Msimu uliomalizika, Diomande alitwaa tuzo ya mchezaji bora kwenye kikosi cha Zoman FC.
"Adebayor anaondoka, nafasi yake inachukuliwa na Diomande, haya yote ni mapendekezo ya kocha, Miguel Gamondi, tunaendelea na usajili, muda si mrefu tutaanika kila kitu hadharani," alisema mtoa taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo.
Awali, winga huyo raia wa Niger, alitakiwa na Simba misimu kadhaa nyuma wakati akiichezea US Gendarmerie ya Niger, ambayo ilimuona kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, 2018.
Mbali na Adebayor, pia Singida Black Stars imethibitisha kuachana na nyota wake Victoria Adebayor, winga Emmanuel Lobota pamoja na Habibu Kiyombo.
Akithibitisha taarifa hiyo Msemaji wa Klabu hiyo, Hussein Masanza, alisema amelazimika kutaja baadhi ya wachezaji wanaoachana nao msimu huu ili kila mmoja akatafute maisha yake mengine.
"Hao ni baadhi ya wachezaji ambao Gamondi [Miguel]amesema hawezi kuendelea nao msimu ujao kwani lengo lake ni kuwa na kikosi imara ambacho kitaonesha ushindani," alisema Masanza.
Alisema ameamua kutoa taarifa hiyo mapema kwa kuwa hao ni miongoni mwa wale ambao hawapo kwenye benchi la ufundi licha ya kuwa na viwango vizuri.
"Nimefanya hivyo ili kila mwananchi pamoja na shabiki wetu afahamu kinachoendelea kwani maneno yamekuwa mengi kwenye mitandao ya kijamii yanayochanganya wachezaji wetu," alisema Massanza.
Singida ni timu ya pili kusajili mchezaji kutoka Zoman FC, ambapo Yanga ilikuwa ya kwanza kwa kumsajili mshambuliaji, Celestin Ecua, anayetarajiwa kutambulishwa hivi karibuni.
Mpaka sasa, Singida imewatangaza rasmi wachezaji wawili, ambao ni Andrew Simchimba kutoka Geita Gold, aliyekuwa kinara wa mabao Ligi cha Champioship, ikipata pia saini ya Kelvin Kijili, beki wa kulia kutoka Simba.
Msimu uliomalizika, Singida ilimaliza kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu, ikikusanya pointi 57, hivyo kupata tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho msimu ujao, huku pia ikifika fainali ya Kombe la FA, kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Yanga, katika mchezo wa fainali, uliopigwa Uwanja wa New Aman Zanzibar.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED