KISHINDO cha matokeo kwa walioomba kuwania nafasi ya Viti Maalum udiwani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimewakumba baadhi ya vigogo wa chama hicho, baada ya wengi wao kukatwa.
Jana, matokeo ya nafasi hizo yalianza kutangazwa katika maeneo mbalimbali nchini na viongozi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT).
Matokeo katika baadhi ya maeneo ya mikoa mbalimbali nchini ni kama yalivyotangazwa:
MOROGORO
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro matokeo ya nafasi ya Viti Maalum udiwani yalihitimishwa jana, huku baadhi ya vigogo maarufu wakiangukia pua.
Kadhalika katika uchaguzi huo madiwani sita wa zamani waliofanikiwa kutetea nafasi zao na kurejea ni Latifa Ganzel, Grace Mkumbae, Salma Mbandu, Warda Bazia, Rahma Maumba, na Amina Zihuye.
Hata hivyo, viongozi maarufu waliokuwa wakitetea nafasi zao za udiwani, akiwamo Hadija Kibati maarufu “Mama Nyau,” Zamoyoni Abdallah, Mwanaidi Ngulungu na Aisha Kitime, wamebwagwa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Uchaguzi huo ulifanyika jana asubuhi, ulimalizika kwa kutangazwa kwa matokeo saa 12:15 asubuhi na msimamizi wa uchaguzi.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Wilaya ya Morogoro Mjini, Khalid King, alisema uchaguzi huo umehitimishwa kwa amani.
Alisema kura zilizopigwa zilikuwa 1,153, kati ya hizo 29 ziliharibika na halali zilikuwa 1,124.
Matokeo ya uchaguzi huo yalitangazwa kuwa Latifa Ganzel, ambaye ni mwandishi wa habari mkoani Morogoro, aliibuka kinara kwa kupata kura 934.
Aliwataja wengine ni Batuli Kifea (794), Grace Mkumbae (752), Salma Mbandu (698), Imakulata Mhagama (581), Warda Bazia (562), Rahma Maumba (560), Magreth Ndewe (556), Anna Kisimbo (535), na Amina Zihuye (532).
Akizungumzia baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Mwenyekiti wa UWT Tawi la Mwere, Anna Hoza alisema uchaguzi huo umefanyika kwa utulivu mkubwa na anaamini ulikuwa huru na haki.
"Tunaomba waliopata kura chache wasikate tamaa, CCM ina nafasi nyingi za uongozi. Tujiandae kwa chaguzi zijazo kwa moyo mpya,” alisema.
Katibu wa UWT Tawi la Nogutu, Marietta Luvunzu, alisema uchaguzi huo umeonesha dira mpya ya nafasi ya wanawake ndani ya siasa za chama na taifa:
“Tumeona jinsi wanawake walivyojitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, watu 31 ambao majina yao yalirejeshwa kati ya wengi waliokuwa wamejitokeza kutia nia, inaonesha kuwapo ushindani wa hali ya juu na uthubutu. Hii ni hatua ya maendeleo ya UWT, CCM na mustakabali wa taifa.” alisema.
Mjumbe wa UWT tawi la Chamwino, Ziada Kondo, alisema wanawake wanaweza na uchaguzi huo umethibitisha hilo.
Alisema UWT Morogoro Mjini imewapa taswira mpya ya namna wanawake wanavyochukuliana kwa heshima na mshikamano.
DAR ES SALAAM
Katika Mkoa wa Dar es Salaam mchakato huo ulifanyika katika halmashauri zote nne. Akitangaza matokeo hayo jana, Katibu wa CCM Wilaya ya Ubungo, Henry Mwenge, alisema Tarafa ya Kawe aliyeibuka mshindi ni Dorice Mrimi, aliyepata kura 847.
Wengine ni Twilumba Balama (734), Wema Kasuga (549) na Lilian Shirima (518) ambao walipigiwa kura na wajumbe 1,720.
ARUMERU
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa UWT Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Esupath Naikara, alisema madiwani 11 wa Viti Maalum kwenye tarafa tatu za wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha wamepenya kwenye kinyang'anyiro cha kura za maoni, kati ya 24 walioomba .
Naikara, alisema idadi ya wajumbe walikuwa 1,168. Huku kura zilizopigwa zilikuwa 1,018, kura zilioharibika 32 na idadi ya kura halali zilikuwa 686.
TARIME
Wilayani Tarime mkoani Mara, kati ya wagombea 55 waliojitokeza kuwania nafasi ya Viti Maalum, Esther Nyarandi kutoka tarafa ya Inano aliongoza kwa kupata kura 944, akifuatiwa na Sophia Mtongori (884).
Uchaguzi wa kuwapata wagombea hao ulisimamiwa na makatibu wa CCM wilaya, Hassan Moshi, Aelin Molel na Katibu UWT Wilaya, Nyasatu Manumbu.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa UWT Wilaya, Nyasatu Manumbu, alisema Luth Samwel alishika nafasi ya tatu (813) na wagombea wawili kutoka tarafa ya Ingwe wakipata kura 405.
Manumbu alisema uchaguzi huo ulimalizika vizuri na kulikuwa na wagombea 55 kutoka tarafa za Ingwe, Inchugu, Inchage na Inano na wote walitia saini matokeo na kwa sasa kinachosubiriwa ni uamuzi kutoka ngazi ya mkoa.
Aliwataja madiwani walioshinda katika Tarafa ya Moshono ni Nina Masanja (871), Happy Zelothe (696), Nai Mollel (474) na Eveline Mollel (432).
Pia, katika Tarafa ya Enaboisho, walioshinda ni Anet Kifwe (797), Grace Seneu (786) na Fauzia Mohamed (489).
Alisema katika Tarafa ya Mukulat ni Asha Said (775), Fafaja Kivuyo (737) na Elinipa Laizer (738).
LINGIDO
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM Wilaya ya Longido, Lekui Solomoni, alisema katika Tarafa ya Enduimet aliyeongoza ni Nalepo Ngolepo Laizer (728), Hellen Elia Laizer (159) Miriam Samwel Laizer (169).
Wengine ni Neema Lee Mamasita (655), Nosotwa Mohono Mollel (363), Witness Naarparakuo Mollel (615), Pesi Lemeek Laizer (85).
Tarafa ya Ketumbein ni Julitha Ernest Anton (253), Beth Karaine Laizer (229), Elizabeth Timotheo Laizer (723), Rehema Kesoi Mollel (463), Nageli Samwel Mollel (546) na Magreth Mika Mollel (551).
Katika Tarafa ya Engarenaibor, Merisiana Edward Bendera (680), Nanyorri Njeri Kakanyi (560), Sayuni Lengulayai Laizer (771), Lucy Lukas Laizer (90) na Sarah Oltetia Mollel (706).
Tarafa ya Longido, Esupat Ngulupa Laizer (459), Esther Lothi Laizer (126), Mary Kuya Mollel (728) Sarah Lazaro Mollel (791) na Upendo Malulu Ndoros (660).
"Mwisho wa uchaguzi huu ni mwanzo wa uchaguzi ujao. Niwaombe wana CCM wote tuungane na tuendelee kuwa wamoja katika kuendelea kuwapendekeza viongozi wanaotokana na chama chetu ili tukawape ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu."
Kadhalika, aliwataka wananchama wa CCM kuendelea kuwa wamoja katika kuhakikisha chama kinaendelea kushika dola wakati wote.
KAHAMA
Akitangaza matokeo ya nafasi ya Viti Maalum udiwani wilayani Kahama, Katibu wa UWT CCM Wilaya, Happynes Charles, alisema Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kahama, Therezia Salia, ameongoza kura za maoni dhidi ya mpinzani wake.
Alisema Salia amepata kura 1,093 na kuongoa Tarafa ya Kahama Mjini.
Uchaguzi ulianza Julai 20 saa moja asubuhi na kukamilika Julai 21, saa 12 asubuhi huku kila mgombea akiridhika na matokeo hayo.
Alisema, Tarafa ya Kahama Mjini Salia aliongoza kwa kupata kura 1,093, akifuatiwa na Vaileth Bulili (1041), Elika Makaga (954), Rehema Joshua (948) na Marry Charles (314).
Katika Tarafa ya Isagehe, Scolastika Kahanya, alipata kura (840), Mpaji Mwali (839) na Winfrida Peter Jumbe (462).
Charles aliijataja Tarafa ya Msalala kuwa ni Mariamu Mkwiwa Ngereja (933), Nyagwema Wariyoba (650), Hamisa Kalinga Miando (567) na Grace Masanja Kabiliga (541).
Tarafa ya Isagehe Msalala akiwa ni Pili Izengo (499), Mwashi Madata (501) na Matha Shedrack (478).
Tarafa ya Dakama Halmashauri ya Ushetu, Betha Leonard (733), Yulitha Msafiri (765), Felister Nyerere Kabasa (767), Maria Maziku (471) na Eva Pius Mkonya (514).
Katika Tarafa ya Mweli ikiongozwa na Asha Marco (1153), Ester Matone (1,042) pamoja na Heleni John (612).
Walioomba nafasi ya udiwani Viti Maalumu walikuwa 90 na walioteuliwa walikuwa 66, kati yao 23 ndio wameshinda nafasi hizo kwa awamu ya kwanza na awamu ya pili wanasubiri ratiba ya vikao vya uteuzi.
*Imeandaliwa na Shaban Njia (Kahama), Cynthia Mwilolezi (Arusha) Samson Chacha (Chacha), Zanura Mollel (Longido) Maulid Mmbaga (Dar) na Ida Mushi (Morogoro)
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED