HOSPITALI YA MKAPA: Mapinduzi ya kikanda, vikwazo vikuu wataalam, maabara zinazohitajika

By Sanula Athanas , Nipashe
Published at 01:13 PM Jul 22 2025
Rais Samia Suluhu Hassan (kulia), akiwekeana ahadi na mmoja wa watoto waliopandikizwa uloto BMH, jijini Dodoma Februari 01, 2024 baada ya Mkuu wa Nchi kuzuru hospitalini huko.
Picha: Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan (kulia), akiwekeana ahadi na mmoja wa watoto waliopandikizwa uloto BMH, jijini Dodoma Februari 01, 2024 baada ya Mkuu wa Nchi kuzuru hospitalini huko.

KATIKA ardhi ya Tanzania, ambapo ugonjwa wa selimundu umekuwa ukitesa jamii kwa miaka mingi, Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma sasa imeibuka kama nguzo ya matumaini.

Hatua kubwa zaidi ni ya Mei mwaka huu. BMH ilitangazwa kuwa Kituo cha Umahiri wa Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Tiba ya Selimundu kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. 

Mnamo Mei 9 mwaka huu, gazeti Daily News linalomilikiwa na Serikali ya Tanzania, liliripoti kuwa tuzo hiyo kwa BMH ilitangazwa wakati wa Mkutano wa 25 wa Mawaziri wa Sekta ya Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Arusha.

Dk. Stella Malangahe, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Damu BMH, anasema wazo la kuanzisha huduma ya upandikizaji uloto BMH lilianza kama jitihada za serikali kukabiliana na madhila ya selimundu.

Bingwa huyo wa Magonjwa ya Damu anasema mipango ilihusisha kusomesha wataalamu, kuboresha miundombinu ya hospitali, na kuanzisha ushirikiano wa kimataifa, hasa katika vipimo vya maabara ambavyo havipo nchini.

Anasema kuwa kwa sasa, BMH haifanyi kazi tu kama hospitali, bali kama lango la matumaini kwa mamilioni ya watoto waliozaliwa na selimundu – si tu Tanzania, bali Afrika Mashariki na Kati.

VIKWAZO VIKUU 

Pamoja na mafanikio haya, changamoto zipo. Dk. Stella anasema upungufu wa wataalamu waliobobea katika upandikizaji uloto ni mkubwa. 

"Huduma ya upandikizaji uloto inahitaji uwe na nesi mbobezi kwa kila mgonjwa, jambo ambalo kwa sasa hatujafikia," anaeleza.

Bingwa Stella anabainisha kuwa kwa sasa, BMH ina mabingwa watano tu wa magonjwa ya damu – mmoja kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na wanne ni watumishi wa hospitali hiyo.

"Wakati tunaanza (mwaka 2023) tulikuwa madaktari wawili tu," Dk. Stella anasema. "Lakini sasa tumeongeza watatu zaidi ndani ya miaka miwili."

Kwa ujumla, Dk. Stella anasema BMH bado ina pengo kubwa la madaktari, manesi, wataalamu wa maabara na wafamasia wenye elimu ya kutosha kuhusu sikoseli na wagonjwa wake. 

Si hilo tu. Tiba ya upandikizaji uloto haiwezi kufanyika bila HLA Compatibility Test – kipimo cha mfanano wa vinasaba kati ya mgonjwa na mtoaji uloto. Tanzania haina maabara ya kiwango hiki. Dk. Stella anasema BMH hutuma sampuli Ujerumani zinakopimwa kwa hisani.

Bingwa huyo anasema HLA Compatibility Test ni kipimo cha hali ya juu kinachoangalia namna vinasaba vinavyofanana. Mfanano huo ndio unaowapa uhakika wa kuota kwa uloto unaopandikizwa. Anafafanua:

"Gharama ya kipimo hiki inakadiriwa kuwa Sh. milioni mbili hadi tatu kwa mtu mmoja. Kumbuka tunapotaka kupandikiza uloto, huwa hatuchukui sampuli za mtu mmoja tu, huwa tunachukua sampuli za ndugu zake wote waliozaliwa naye tumbo moja. 

"Kama unavyojua familia zetu za Kiafrika, mnaweza kuwa watoto mpaka saba. Kwa hiyo, kufanya kipimo hiki inaweza kugharimu hadi Sh. milioni 21 kwa familia moja yenye watoto saba," anaeleza Dk. Stella na kuongeza: 

"Maabara hii ya Ujerumani imetupunguzia gharama maradufu kwa sababu inapima sampuli bila malipo yoyote kutoka kwetu. Tunatuma sampuli kwa njia ya DHL."

FEDHA ZA UMMA

Wakati changamoto hizi za rasilimali watu na miundombinu zikiendelea kuisonga BMH, ripoti mpya zinaonesha kuwa fedha ambazo zingeweza kutatua kabisa matatizo haya zipo, lakini zimepotea au ziko hatarini kupotea.

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Sh. trilioni 11.857 zimeripotiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa hatarini kupotea kutokana na viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu. 

Hii ni kwa mujibu wa uchambuzi wa ripoti za CAG uliofanywa na Taasisi ya WAJIBU, inayoongozwa na CAG mstaafu Ludovick Utouh – mwanazuoni wa uhasibu.

Taasisi            2019/20          2020/21 2021/22        2022/23

Serikali Kuu    Bil 560.19/-     Bil 1,781.77/-              Bil 770.91/-     Bil 676.66/-

S/Mitaa          Bil 863.85/-     Bil 1,400.60/-              Bil 297.86/-     Bil 499.96/-

Mashirika       Bil 346.80/-     Bil 1,408.36/-              Bil 2,015.78/-  Bil 1,234.67/-

Jumla             Bil 1,770.84/-Bil 4,590.73/-               Bil 3,084.55/-Bil 2,411.29/-

Mwenendo wa viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2022/23. CHANZO: Ripoti ya Uwajibikaji 2022/23 ya Taasisi ya WAJIBU. Uk. 4

Je, fedha hizi zingefanyiwa matumizi sahihi, zingewafanya watoto wengi zaidi wenye selimundu kupona? Bila shaka. Kwa mfano:

Sh. bilioni tatu tu zinaweza kugharamia vipimo vya ufanano wa vinasaba (HLA Compatibility Test) kwa familia elfu moja (1,000), ambavyo kwa sasa Tanzania hulazimika kutuma sampuli Ujerumani zinakopimwa kwa hisani.

Sh. bilioni tano zinaweza kutosha kuajiri na kutoa mafunzo kwa manesi 100 waliobobea katika tiba ya selimundu, kila nesi akigharimu Sh. milioni 50.

Sh. bilioni 10 zingejenga hosteli ya wagonjwa na ndugu zao, ambayo sasa kwa BMH bado ni ndoto iliyo kwenye karatasi.

Kwa jumla, robo tu ya hizo Sh. trilioni 11.857 ingetosha kuipanua BMH kuwa kituo cha tiba ya selimundu kwa kiwango cha kimataifa – chenye uwezo wa kuhudumia maelfu ya wagonjwa kutoka Afrika nzima, bila kutegemea msaada wa nje.

Fedha hizo zingeweza kubadilisha taswira ya huduma za afya nchini – si kwa BMH pekee, bali pia kwa hospitali nyingine nyingi za rufani na mikoa. Zingewezesha kutoa ajira, vifaa tiba na dawa muhimu, lakini sasa zinatajwa katika orodha ya upotevu.

Katika taifa ambalo linapoteza zaidi ya Sh. trilioni 11 kutokana na udanganyifu, ubadhirifu na rushwa, BMH inathibitisha kwamba mabadiliko yanawezekana, endapo fedha za umma zitatumika ipasavyo. 

‘VUNJA MDUARA’

Mbali na matibabu, BMH inashirikiana na Wizara ya Afya kuzuia vizazi vijavyo vya wagonjwa wa selimundu kupitia kampeni ya kitaifa “Vunja Mduara wa Sikoseli.” 

Huu ni mpango unaohamasisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupima hali zao kabla ya kuingia katika maisha ya uzazi.

"Ujue hali yako mapema. Ukijua una vinasaba vya sikoseli, unashauriwa kutopata mtoto na mwenzio mwenye hali kama yako," Dk. Stella anasisitiza. "Hii ndiyo njia pekee ya kuzuia ugonjwa huu kwa vizazi vijavyo."

Kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 (Toleo la 2023), elimu ya msingi na sekondari ni ya lazima kwa watoto wote nchini. Endapo kampeni ya "Vunja Mduara wa Sikoseli" itawafikia wanafunzi wote nchini, kila mmoja atapata uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa wa sikoseli, hivyo kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo nchini.

Kukabiliana na selimundu nchini, Meneja wa Kitengo cha Maradhi Yasiyoambukiza - Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Omar Muhammed Suleiman, anashauri serikali kutenga bajeti maalum ya selimundu ikihusisha utafiti, utoaji elimu kwa wananchi na upandikizaji uloto kwa watoto wanaougua ugonjwa huo.

Dk. Suleiman, ambaye ni Bingwa wa Maradhi ya Moyo kwa Watoto, anasema: "Eneo lingine tunalotakiwa kuwekeza kama nchi ni kusomesha vijana wa kutosha ili tuwe na wataalamu wengi katika hospitali zetu."

KUHUSU BMH

Kwa mujibu wa Msemaji wa BMH, Jeremiah Mbwambo, hospitali hii izinduliwa rasmi tarehe 13 Oktoba 2015. Iko katika kata ya Ng'ong'ona karibu na UDOM, umbali wa Km 10 kusini -mashariki mwa Mji wa Dodoma.

Mbwambo anasema wazo la kujenga hospitali lilitolewa na Jakaya Kikwete. Rais huyu wa Awamu ya Nne ndiye alipendekeza pia jina la kituo hiki cha tiba kinachohudumia zaidi ya watu milioni 14.

"Mbali na tiba ya selimundu, hospitali inatoa pia huduma za upandikizaji mimba, figo na uume, upasuaji moyo na ubongo, mionzi ya saratani na tiba ya nyuklia," Mbwambo anasema.

Anaeleza kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ndiyo ulitoa Sh. bilioni 129 kujenga majengo ya hospitali pamoja na vifaa tiba, zikiwamo mashine za X ray na CT-Scan yenye thamani ya Sh. bilioni 1.6 iliyoanza kutumika mwaka 2017.