KLABU ya Tabora United, imedaiwa iko katika hatua za mwisho kumalizana na kiungo mkabaji Palai Manjie, raia wa Cameroon, kurithi mikoba ya Nelson Munganga, anayetimkia Dodoma Jiji.
Habari kutoka ndani ya Klabu ya Tabora United, zinasema kuwa wawakilishi wa mchezaji huyo wapo jijini Dar es Salaam kukamilisha dili la mchezaji huyo kujiunga na timu hiyo.
Kiungo huyo anakuja kuziba nafasi ya Munganga, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, anayedaiwa kumalizana na Dodoma Jiji, ambapo aligomea mkataba mpya na kuamua kutafuta changamoto sehemu mpya.
"Ni kweli, Tabora United inaongea na wawakilishi wa mchezaji huyo, tena si huyo tu, pale Ukonga kuna hoteli moja hivi wamejazana wachezaji wengi kutoka Nigeria, kila kitu kinafanyika pale, wamekuwa wakifanya mazungumzo na wachezaji kadhaa hapo," alisema mtoa taarifa.
Alisema kuwa viongozi wa Tabora United wanatarajia kutangaza majina na wachezaji waliowaacha na kuwasajili wiki ijayo, huku suala la maandalizi ya msimu likiratibiwa.
Tabora United ilimaliza nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliomalizika ikikusanya pointi 38.
Hata hivyo, timu hiyo ambayo ilitumia makocha wanne mpaka kumaliza msimu, ilipata mafanikio makubwa ilipokuwa na Anicet Kiazayidi, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambaye taarifa zinasema kwa sasa anamalizana na Dodoma Jiji ili kuwa kocha mkuu badala ya Mecky Maxime, ambaye anarejea kukinoa kikosi cha Mtibwa Sugar.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED