Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inatarajia kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za ununuzi wa hewa tiba ya oksijeni, ambazo awali zilifikia Shilingi milioni 9 kwa mwezi, kufuatia ujenzi wa mradi mpya wa kufua hewa tiba na usimikaji wa mitambo utakaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 1.439.
Akizungumza leo, Julai 22, 2025, mara baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi la mradi huo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. David Mwasota, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa chini ya Wizara ya Afya kwa ufadhili wa Global Fund, na umelenga kupunguza utegemezi wa hospitali hiyo kwenye mikoa ya Dodoma na Manyara kwa ajili ya kupata hewa tiba.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukinunua oksijeni kutoka nje ya mkoa, hali iliyosababisha gharama kubwa za uendeshaji. Kukamilika kwa mradi huu kutapunguza mzigo huo na kuimarisha huduma za afya kwa wagonjwa wetu,” alisema Dkt. Mwasota.
Mradi huo utakapokamilika, unatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa oksijeni ya kutosha kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura, chumba cha upasuaji, wagonjwa wa mfumo wa upumuaji, pamoja na vitengo vya ICU na watoto wachanga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED