Dk. Yonazi: Tanzania ikotayari kwa CHAN 2025

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 01:49 PM Jul 22 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi, (kulia) wakati akikagua miundombinu itakayotumika katika mashindano ya CHAN.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi, amesema kuwa Tanzania iko tayari kwa ajili ya kuandaa Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), yanayotarajiwa kuanza rasmi Agosti 2, mwaka huu.

Akizungumza jana baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa miundombinu ya michezo jijini Dar es Salaam, Dk. Yonazi amesema maandalizi yamefikia hatua nzuri na viwanja viko tayari kwa mashindano hayo makubwa Afrika.

Dk. Yonazi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Makatibu Wakuu ya CHAN na AFCON, amekagua viwanja vya Benjamin Mkapa, Isamuhyo, Shule ya Sheria na Gymkhana.

Uwanja wa Benjamini Mkapa
“Nisisitize kwamba serikali imejipanga vizuri kuhakikisha miundombinu yote ya michezo itakayotumika katika michuano hiyo inakidhi viwango vya kimataifa,” amesema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, ametoa wito kwa Watanzania kuonesha uzalendo kwa kujitokeza kwa wingi viwanjani kuishangilia timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’.