CCM yaja na QR Code kukabili taarifa potoshi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:37 PM Jul 21 2025
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.
Picha: Mtandao
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amesema chama hicho kimesema kimeanza matumizi ya QR Code maalum kwa ajili ya kusaidia wananchi kuhakiki na kutambua taarifa rasmi zinazotolewa na CCM.

Amesema kuwa hatua hiyo ni kukabiliana na mapambano dhidi ya wimbi la uzushi na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na watu wenye nia ovu ya kuchafua taswira ya chama na kuleta taharuki katika jamii.

Kwa mujibu wa Makalla, kupitia QR Code hiyo, msomaji anaweza kufanya scan kwa kutumia simu ya mkononi na moja kwa moja kupelekwa kwenye taarifa rasmi iliyowekwa kwenye tovuti au kurasa za mitandao ya kijamii ya chama. Endapo taarifa husika ni ya uongo, scan ya QR Code hiyo haitaleta chochote au itapeleka kwenye taarifa rasmi inayobainisha uongo wa taarifa husika.

“Mfano mzuri ni taarifa ya uzushi iliyotengenezwa na kusambazwa tarehe 20 Julai 2025, ambayo chama kiliikanusha. Msomaji aki-scan QR Code ya CCM, atapelekwa kwenye taarifa rasmi iliyo na kichwa kisemacho: ‘CCM YATOA RAMBIRAMBI KWA AJALI YA GARI – IWAMBI, MBEYA’ jambo linalothibitisha kuwa taarifa iliyosambazwa awali ilikuwa ya kupotosha,” amesema Makalla.

Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kuwahimiza Watanzania na walaji wote wa habari kuhakikisha wanathibitisha uhalali wa taarifa wanazopokea kwa kutumia mfumo huu, ili kujiepusha na upotoshaji unaoweza kuathiri utulivu wa taifa na mshikamano wa kijamii.

CCM inasisitiza kuwa njia sahihi ya kupata taarifa zake rasmi ni kupitia vyanzo vilivyohakikiwa kwa QR Code na kwamba yeyote anayehitaji kujiridhisha kuhusu ukweli wa taarifa yoyote inayodaiwa kutoka CCM, anaweza kufanya hivyo kwa urahisi na haraka kwa kutumia teknolojia hii.