Askofu Shoo azungumza mazito uchaguzi mkuu

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:13 PM Oct 18 2025
Askofu Dk. Frederick Shoo akiwa katika mkutano mkuu wa 17 wa Jimbo la Kilimanjaro Kati la KKKT.
PICHA: GODFREY MUSHI
Askofu Dk. Frederick Shoo akiwa katika mkutano mkuu wa 17 wa Jimbo la Kilimanjaro Kati la KKKT.

ASKOFU wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo, amesema ni makosa kuacha kujitokeza kushiriki kupiga kura, huku akiwataka Watanzania wasikubali mtu yeyote awaondolee haki na wajibu wao wa kuchagua kiongozi wanayemtaka.


Akizungumza leo (Oktoba 18, 2025) katika Mkutano Mkuu wa 17 wa Jimbo la Kilimanjaro Kati la Dayosisi hiyo uliofanyika Majengo, Moshi, mkoani Kilimanjaro, amesema hoja inayoendelea ya watu kuacha kuona umuhimu wa kushiriki mchakato wa uchaguzi, hayo ni makosa.

"Wito wetu wote tunapoingia katika uchaguzi mkuu, tuombee mchakato mzima. Na sisi tumewahamasisha watu washiriki na kujitokeza kikamilifu katika kupiga kura.

Sisi tutambue tunao wajibu wa kuchagua, tena wajibu wa kikatiba. Tusikubali mtu yeyote atuondolee haki yetu na wajibu wetu, tusikubali. Mungu anataka tushiriki, tufanye uchaguzi, tusimame kama raia na wananchi tukachague viongozi tunaowataka.

"Kubwa ni kuhakikisha kwamba nchi yetu, uchaguzi hasa siku ya kupiga kura ufanyike kwa amani, sio matusi na sio watu kupigwa, watu kuumizwa au kuumizana, lakini ufanyike kwa amani na utaratibu.

...Sisi tunazidi kuombea jambo hili kwa sababu nchi hii ni nchi yetu sote. Pasipo amani ni uongo. Hata shughuli zetu zingine tusijidanganye hazitaweza kufanyika. Kwa hiyo tuhakikishe kwamba shughuli hii inakwenda kumalizika salama."

Aidha Askofu Shoo amesisitiza: "Kwa hiyo mimi ningelisema sababu zozote zile zinazoweza kuleta machafuko katika mchakato mzima huu wa zoezi hili la kuchagua viongozi wetu, nafikiri hizo tuna uwezo wa kuzikataa. Kwa sababu tunataka uchaguzi wa amani ulio huru na wa haki. Mungu atusaidie sana.

...Kwa sababu tunataka uchaguzi wa amani ulio huru na wa haki. Mungu atusaidie sana.Na wewe (Mkuu wa Wilaya), nikutakie afya njema pamoja na Mkuu wetu wa Mkoa, na hata Rais wetu; kwani bado ni Rais wetu. Hata katika kampeni zake  au Mwenyekiti wa chama, ni Rais wetu na hilo tunaliheshimu na lazima tuliheshimu."

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, akitoa salaam zake katika mkutano huo, amewaomba wajumbe wa mkutano huo, kuwa mawakala wazuri wa kuhakikisha watu wanatimiza haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka. 

"Lakini pia yapo maneno maneno yanatajwa mitandaoni huko na hususani vijana wenzetu.Kuna watu wanasema sisi tutatoka, wengine wanasema sisi tutatiki. Sasa kwa mujibu wa utaratibu watu wanatakiwa kwenda kupiga kura.

Zaidi ameongeza, "Na sisi serikali tutahakikisha kila mmoja anaipata haki yake ya msingi, kwamba hakutakuwa na mtu ambaye atasukumwa, wala ataghasiwa ili aende akapige kura kwa amani na utulivu.

...Liko jukumu ambalo serikali tumepewa lakini pia sisi wa rohoni tuendelee sana kumsihi Mwenyenzi Mungu kuomba amani, utulivu na usalama wa kutosha kipindi hiki ambacho tunaelekea kwenye uchaguzi na hata siku ya kupiga kura na hata baada ya hapo."