DUCE yaipongeza Serikali kupeleka mradi wa 'HEET'

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 10:46 AM Oct 18 2025
DUCE yaipongeza Serikali kupeleka mradi wa 'HEET'
PICHA: PILLY KIGOME
DUCE yaipongeza Serikali kupeleka mradi wa 'HEET'

Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam(DUCE) kimejivunia Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupeleka Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi(HEET) chuoni hapo na kuwaletea mafanikio makubwa.

Kwa kupitia mradi huo unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu unaofadhiliwa na Benki ya Dunia chuo kimeweza kupata dola za Kimarekani Milion nane(8) sawa na TSh. Bil.19 zilizotolewa katika awamu hiyo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. 
Hayo yamesemwa Oktoba 17,2025 na Rasi wa Chuo hicho, Prof. Stephen Maluka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Prof.Maluka amesema kuwa fedha hizo zimeleta mageuzi makubwa sana ndani ya chuo hicho kitaaluma na kuweza kujenga majengo makubwa mawili yenye ghorofa tatu tatu yenye kuwezesha kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji yatakayokuwa na maabara mbalimbali za kisayansi kwa masomo ya kikemia,fizikia,biolojia na mengine yanayohusiana na sayansi.

Kati ya hayo jengo moja litakuwa ni eneo la kuboresha huduma za ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi na wafanyakazi wenye mahitaji maalumu na litakuwa na vifaa vyote vya kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum.

1


Aidha wameweza kufanya ukarabati kwa majengo ya zamani, wameweza kuboresha miundombinu ya TEHAMA kutoka mifumo ya kizamani na kujenga miundombinu ya kisasa.

Aidha wameweza kuboresha maabara na maktaba kuwa za kidigitali na kuboresha miundombinu kuwa ya kisasa kwa kiwango cha juu.

Kupitia mradi huo ndani ya miaka mitatu chuo wamepata ajira mpya zaidi ya 237 ambao wanataaluma na wasio wanataaluma Naibu     Rasi(Taaluma,Utafiti na Ushauri Elekezi) Prof.Amani Lusekelo amesema kupitia mradi huo wanataaluma wameweza kujengewa uwezo na kukuza taaluma kwa kiwango kikubwa.

2


Ikiwemo walimu kupatiwa mafunzo maalum namna ya kutoa adhabu kandamizi na shurutushi kwa wanafunzi na kutakiwa kutoa adhabu mbadala.

Amefafanua mafaniko mengine ni kuanzisha mitaala mipya 12 iliyoboreshwa iendane na soko la dunia na yenye kuangaliwa matakwa ya jamii, nchi na kuendana na dira 2050.

Kwa upande wake Naibu RASI Mipango, Fedha na Utawala pia Mratibu wa Mradi wa HEET(DUCE) Prof.Pendo Malangwa amesema kwa kupitia mradi huo chuo hicho kimeweza kumaliza changamoto kubwa hasa za miundombinu ya majengo yakiwemo madarasa.

“ Tumejivunia mradi huu awali mazingira ya kazi yalikuwa magumu lakini kupitia mradi huu tumeona mabadiliko makubwa sana hasa katika utumishi wa umma”amesema