Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Pangani na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amechukua fomu ya kugombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Aweso amepokea fomu hiyo leo, Agosti 26, 2025, kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Pangani, Juma Bwela, katika hafla iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi na wajumbe wa CCM waliomsindikiza.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Aweso amewaomba wanachama na wananchi wa Pangani kuendelea kujitokeza kwa wingi kusaka kura za CCM, akisisitiza kuwa ushindi wa chama hicho utakuwa heshima kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Hakuna demokrasia ya kupata viongozi zaidi ya uchaguzi. Kwa hiyo niwaombe ndugu zangu wa Chama Cha Mapinduzi na Wanapangani, hatujamaliza uchaguzi, twendeni tukazisake kura za CCM, kura za heshima kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Aweso.
Aweso pia amebainisha kuwa moja ya changamoto kubwa iliyodumu kwa miaka mingi katika jimbo hilo ni barabara ya Tanga–Pangani–Saadani–Bagamoyo, lakini chini ya uongozi wa Rais Samia changamoto hiyo imeanza kushughulikiwa kwa kuanza ujenzi wa barabara na daraja. Alisema utekelezaji huo ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa CCM Pangani na wananchi waliohudhuria walieleza dhamira yao ya kuendelea kumpa kura Aweso, wakimtaja kama kiongozi mchapakazi mwenye dira ya maendeleo, huku wakibainisha mchango wake katika sekta ya maji, elimu na utoaji mikopo kwa wanawake, vijana na wenye uhitaji maalumu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED