Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimesema utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (Higher Education for Economic Transformation – HEET Project) kimeanza kuleta matokeo chanya yatakayokifanya chuo hicho kuwa kitovu cha uzalishaji wa madaktari bingwa na wataalamu wa afya wa ngazi ya juu nchini Tanzania.
Kupitia mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa mkopo wa masharti nafuu, MUHAS kimepata dola za Kimarekani milioni 45.5 (takribani shilingi bilioni 120) zinazotumika katika ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya kufundishia, kujifunzia na kufanya tafiti za afya katika Kampasi za Mloganzila na Kigoma.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa ujenzi wa Ndaki ya Tiba katika Kampasi ya Mloganzila umefikia asilimia 50, huku ujenzi wa Kampasi mpya ya Kigoma ukiwa asilimia 35.
Amesema ujenzi wa Ndaki hiyo ulianza Desemba 2024, ukitekelezwa na wakandarasi Mohammedi Builders Ltd na Hainan International Ltd, chini ya usimamizi wa mshauri elekezi ARQES AFRICA, na unatarajiwa kukamilika Juni 2026.
Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa kumbi za mihadhara zenye uwezo wa wanafunzi 1,400, maabara 21 za kufundishia, bweni la wanafunzi 320, bwalo la chakula, jengo la maktaba na TEHAMA, pamoja na jengo la anatomia na uwanja wa mpira wa miguu.
Kwa upande wa Kampasi ya Kigoma, ujenzi unatekelezwa na China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation Co. Ltd, chini ya OGM Consultants, na unatarajiwa pia kukamilika Juni 2026.
Kutatua changamoto ya upungufu wa wataalamu wa afya
Prof. Kamuhabwa amesema kukamilika kwa mradi huu kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa wataalamu wa afya nchini, hasa madaktari bingwa na wataalamu wa fani adimu kama ganzi, tiba mazoezi, afya kazini, na viungo bandia.
Kwa sasa, kutokana na ufinyu wa miundombinu, MUHAS huchukua mwanafunzi mmoja kati ya 31 wanaoomba nafasi za masomo ya tiba.
Kwa mfano, katika mwaka wa masomo 2025/2026, kati ya waombaji 5,395 wenye sifa za kusoma udaktari wa binadamu, walioweza kujiunga ni 235 pekee, huku katika shahada ya ufamasia, kati ya waombaji 4,972, ni 110 pekee waliopata nafasi.
“Mradi wa HEET utapunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la upungufu wa nafasi za udahili na kuongeza uwezo wa chuo kutoa wataalamu wengi zaidi wa afya kila mwaka,” amesema Prof. Kamuhabwa
Mitaala mipya na tafiti bunifu kuimarisha ubora wa elimu
Ameongeza kuwa kupitia HEET, MUHAS imefanya maboresho ya mitaala 83 na kuanzisha mitaala mipya 23, yote ikiwa na lengo la kuendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya afya na maendeleo ya teknolojia ya tiba duniani.
Chuo pia kimeongeza uwekezaji katika taaluma za utafiti na ubunifu, ambapo zaidi ya wahadhiri 33 wamepelekwa kusoma ngazi za uzamili na uzamivu ndani na nje ya nchi ili kuongeza uwezo wa kufundisha na kufanya tafiti za kisayansi.
"Uwekezaji huu unatarajiwa kulifanya MUHAS kuwa chuo kinachozalisha wataalamu wa afya wa kimataifa, chenye uwezo wa kufanya tafiti za kisayansi zitakazosaidia Taifa kukabiliana na changamoto za magonjwa ya milipuko, afya ya umma, na ubunifu wa tiba za kisasa." amesema Prof. Kamuhabwa
Kampasi ya Kigoma kuwa kitovu cha afya kanda ya magharibi
Kwa upande wa Kampasi ya Kigoma,Prof. Kamuhabwa amesema kuwa kampasi hiyo itakuwa chachu ya maendeleo ya elimu na afya katika ukanda wa magharibi mwa Tanzania, eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa na changamoto ya upatikanaji wa wataalamu wa afya.
“Kupitia chuo hiki kipya, tutazalisha wataalamu watakaoboresha huduma katika hospitali za Kigoma, Rukwa, Katavi na Kagera, na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda Bugando au Benjamin Mkapa,” amesema Prof. Kamuhabwa
Amesisitiza kuwa kampasi hiyo pia itakuwa na maabara maalum za tafiti za magonjwa ya milipuko kama Ebola, Marburg na magonjwa mengine yanayohatarisha afya ya umma, kutokana na ukaribu wa kijiografia na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kuhusu Mradi wa HEET
Mradi wa HEET ulizinduliwa tarehe 13 Juni 2021 na unatekelezwa na taasisi zote za elimu ya juu nchini kwa uratibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mradi huu una malengo saba makuu, yakiwemo:- Kuboresha miundombinu na mifumo ya kujifunzia na kufundishia;
- Kuhuisha mitaala na mbinu za ufundishaji;
- Kuboresha tafiti na bunifu;
- Kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi;
- Kuendeleza TEHAMA katika elimu ya juu;
- Kukuza mapato ya ndani ya taasisi;
- Kuimarisha uwezo wa kufundisha na utawala.
Kupitia utekelezaji wake, HEET inalenga kugeuza taasisi za elimu ya juu nchini kuwa injini ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia, sambamba na kuongeza ufanisi katika kuzalisha wataalamu wanaojibu mahitaji ya soko la ajira.
Serikali ya Awamu ya Sita yapongezwa
MUHAS imetoa pongezi za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono makubwa katika kuboresha elimu ya juu na afya nchini.
“Uwekezaji huu ni ishara ya dhamira ya Rais Samia kuhakikisha Tanzania inakuwa na rasilimali watu ya kutosha na yenye ubora, hususan katika sekta ya afya,” amesema Prof. Kamuhabwa
Vilevile, chuo kimeishukuru Benki ya Dunia, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na viongozi wa mikoa ya Dar es Salaam na Kigoma kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa Taifa.
Kukamilika kwa mradi wa HEET katika MUHAS kutaiweka Tanzania katika nafasi bora ya kuzalisha wataalamu wa afya wa kiwango cha kimataifa, na hivyo kupunguza utegemezi wa madaktari bingwa kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Menejimenti ya chuo hicho:
“Tunapotekeleza dira yetu ya Kutoa mafunzo bunifu ya afya, kufanya tafiti zenye tija, na kutoa huduma bora kwa kutumia teknolojia na ubunifu, tunaamini MUHAS itabaki kuwa kitovu cha ubora wa elimu ya tiba Afrika Mashariki.”