NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amesema Tanzania ina umeme wa kutosha baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa ya uzalishaji umeme, ukiwamo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP ), ambao pekee unazalisha Megawati 2,115.
Naibu Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, Julai 10, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua ya miradi ya kuzalisha umeme, kwa kutumia gesi asilia ya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II, jijini Dar es Salaam.
Amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na TANESCO, baadhi ya maeneo yalikabiliwa changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka sasa yameendelea kuimarika.
Biteko amefafanua kuwa upatikanaji wa umeme unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu na TANESCO, inatarajia kuongeza uzalishaji umeme katika Kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati 1,000.
Aidha, Naibu Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TANESCO kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.
“Kuna maboresho makubwa yamefanyika katika kuwahudumia wananchi naona jitihada kubwa zinafanyika, mmekuwa na uharaka wa kushughulikia changamoto za umeme lakini pia niwapongeze kwa kuimarisha kituo cha miito ya simu sasa wananchi wanahudumiwa bila gharama yoyote,’’ amesisitiza Dk. Biteko.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ameongozana na viongozi mbalimbali, akiwamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED