DAWASA yaikera CCM, Makalla awapa angalizo

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 07:03 AM Jul 15 2024
Katibu wa NEC -Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla.
Picha: Mtandao
Katibu wa NEC -Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla.

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imemkera Katibu wa NEC -Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla:

Wananchi waliolipa fedha kuunganishiwa maji na mamlaka hiyo, hawajapatiwa huduma hiyo kwa muda mrefu.

Makalla amesema alipata malalamiko kuhusu ugawaji vifaa kwa wananchi waliolipia maji, lakini baada ya kusikia atafanya ziara huko wamewahi kwa kuanza kuvigawa.

Amesisitiza kuwa hatopenda kuona tena yaliyotokea wiki iliyopita mpaka wasukumwe na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na mabadiliko aliyofanya ndipo wafanye kazi.

Makalla aliyasema hayo jana wakati akikagua mradi wa tangi la maji la Mshikamano, wilayani Ubungo, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Makalla pia alitembelea shule ya sekondari ya mchepuo wa sayansi (Dar es Salaam Girls High School) iliyoko wilayani Ubungo ambayo ni miongoni mwa zinazojengwa kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na kuwataka wanafunzi kutimiza ndoto ya Mkuu wa Nchi kwa kutopata mimba au kuwa watoro.

Akiwa kwenye mradi wa maji, Makalla alisema wakati huo walipompa taarifa Rais Samia kuhusu historia ya maji mkoani humo, upatikanaji wake ulikuwa wa asilimia 90 na kuagizwa itafsiriwe ili walioko pembezoni mwa mji wajue nao ni sehemu ya mkoa huo.

Alisema Rais Samia alipotoa fedha za UVIKO-19 zilipelekwa pia katika mradi huo ili wananchi wapate huduma ya maji.

"Maelekezo ya CCM ni kuhakikisha wananchi wanapata maji. Kazi tunayowaachia mmeniambia eneo lililobaki kupata maji Jimbo la Kibamba ni Msumi.

"Mmeeleza mnachimba visima vitatu na mna mpango wa muda mrefu wa kujenga tangi, ufanyike haraka wananchi wapate maji.

"Watendaji mkianza kulegea hamjui pampu kama zinafanya kazi, hamjui kama maji yanaingia katika tangi wala kama wananchi wanapata maji, hilo ni tatizo," alisema.

Makalla aliagiza wananchi wanapolipa ili kuunganishiwa maji wasicheleweshewe, wapatiwe huduma haraka.

Awali Mbunge wa Kibamba, Issa Mtemvu, alisema eneo ambalo halijapata maji jimboni humo ni Kata ya Mbezi, Mtaa wa Msumi.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ubungo, Rogati Mbowe, alisema Waziri Aweso amefanya "maajabu makubwa Ubungo" na wananchi wamefurahi kwa kuwa walikuwa wanapigwa danadana.