Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Halima Okash, amewahakikishia wakazi wa wilaya hiyo usalama wa kutosha katika kipindi cha kuelekea na siku ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na wananchi, Okash alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimeimarishwa ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.
Amesema wazee na watu wenye mahitaji maalumu watapewa kipaumbele watakapofika kwenye vituo vya kupigia kura, ili waweze kutekeleza haki yao ya kikatiba bila usumbufu.
“Ulinzi na usalama umeimarishwa kuelekea siku ya kupiga kura. Wananchi wanatakiwa kutembelea vituo vyao na kuhakikisha majina yao yapo kwenye orodha ya wapiga kura,” alisema Okash.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, Chemba ina jumla ya vituo 519 vya kupigia kura vilivyogawanyika katika kata 26, ambavyo vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi jioni.
Aidha, amewakumbusha wananchi kuzingatia muda na kufuata maelekezo ya Tume ya Uchaguzi, ikiwemo utaratibu wa utambuzi kupitia vitambulisho halali vitakavyotumika siku ya kupiga kura.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED