DCEA yatoa pendekezo wauza dawa za kulevya kunyongwa, yawataka kujisalimisha

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 07:55 PM Oct 03 2025
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo.
Picha: Mtandao
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeeleza kuwa ipo tayari kushauri mamlaka husika kutunga sheria itakayoruhusu wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya nchini kunyongwa.

Pamoja na pendekezo hilo, mamlaka imewataka watu wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kujisalimisha na kuwaomba radhi Watanzania kwa kosa hilo. 

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mamlaka iko tayari kuwasamehe watakaofanya hivyo kwa hiari na kutoa ushirikiano wa dhati.

“Yeyote anayetaka kujisalimisha afike ofisi za mamlaka au apige namba 119 ili apatiwe maelekezo zaidi. Mamlaka haitawachukulia hatua za kisheria watakaojitokeza na kuwaomba radhi wananchi,” alisema Kamishna Lyimo.

Aliesema dawa za kulevya zina athari kubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla, ikiwemo kuchochea uhalifu unaofanywa na waraibu na kuharibu miundombinu ya maendeleo ambayo imegharimu fedha nyingi za umma.

Aliongeza kuwa wauzaji wa dawa hizo wanapaswa kuwaomba radhi Watanzania kwa madhara makubwa waliyosababisha.

“Wapo walioko mafichoni ndani ya nchi  nawaomba wajitokeze. Kwa wale waliokimbilia mataifa jirani, tunafahamu wapo nchi zipi na tunaendelea kushirikiana na nchi hizo ili kuwapata na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema Kamishna Lyimo.

Kamishna Lyimo alitoa kauli hiyo wakati wa zoezi la uteketezaji wa dawa za kulevya zenye uzito wa jumla ya kilogramu 4,402.02 za aina mbalimbali zilizokamatwa nchini. Zoezi hilo lilifanyika katika kiwanda cha saruji cha Twinga kilichopo Wazo, jijini Dar es Salaam.

Alizitaja dawa zilizoteketezwa kuwa ni pamoja na kilogramu 2,168.18 za methamphetamine, kilogramu 1,064.29 za heroin, gramu 326.95 za cocaine, kilogramu 515.48 za bangi, na kilogramu 653.74 za mirungi.

Ameeleza kuwa dawa hizo zilihifadhiwa kama vielelezo katika mashauri mbalimbali yaliyoko mahakamani, ambapo baadhi ya mashauri bado yanaendelea kusikilizwa huku mengine yakiwa tayari yametolewa hukumu,Kwa mashauri ambayo hayajakamilika, mahakama iliagiza dawa hizo kuteketezwa kutokana na hatari ya kuharibika au kubadilika umbo.

Hatua hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, ambayo inaelekeza vielelezo vya dawa za kulevya kuharibiwa wakati shauri likiendelea au baada ya hukumu kutolewa.

Miongoni mwa mashauri yaliyohusiana na dawa zilizoteketezwa ni kesi ya Najim Abdallah Mohamed, iliyohusisha heroin kilogramu 882.71 na methamphetamine kilogramu 2,167.29.

Aidha, mashauri yaliyotolewa hukumu ni pamoja na ya Hassan Azizi, Salum Shaaban Mpangula, na Hemed Juma Mrisho maarufu “Hororo”, ambao walihukumiwa kifungo cha maisha. Wengine ni Ramadhan Shaban Gumbo aliyehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Irene Dickson Mseluka aliyehukumiwa miaka mitano jela, na Gema Victor Mmasy aliyehukumiwa miaka mitatu jela.

Kamishna Lyimo alisisitiza kuwa mamlaka itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kiutendaji ili kuhakikisha Tanzania inalindwa dhidi ya madhara ya dawa za kulevya.