TARURA kusitisha mikataba ya makandarasi wasiotekeleza miradi Rufiji

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 09:30 PM Oct 03 2025
TARURA kusitisha mikataba ya makandarasi wasiotekeleza miradi Rufiji
Picha: Mpigapicha Wetu
TARURA kusitisha mikataba ya makandarasi wasiotekeleza miradi Rufiji

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Pwani uko katika hatua za kusitisha mikataba ya makandarasi wawili wa kampuni ya HariCom International Ltd na Trinity Manufacturing Services, baada ya kushindwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara kwa wakati.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, amebainisha hayo wakati wa ziara yake ya kikazi Rufiji, ambapo alikagua utekelezaji wa miradi ya barabara inayoendelea wilayani humo.

Amesema makandarasi hao walishinda zabuni na kulipwa malipo ya awali, lakini wameshindwa kutekeleza mikataba yao.

 “Kampuni ya HariCom International Ltd ilipata zabuni ya ujenzi wa barabara ya Polisi–Kirungi yenye urefu wa kilomita moja. Walilipwa shilingi milioni 160 kama malipo ya awali, lakini mpaka sasa hawajafanya kazi yoyote na wameacha vifaa vyao katika eneo la mradi. Gharama ya mradi huo hadi kukamilika ilikadiriwa kufikia shilingi bilioni 1.07,” alisema Mativila.

Kwa upande wa kampuni ya Trinity, alisema walipatiwa malipo ya awali ya shilingi milioni 460 tangu Agosti mwaka jana, na mradi wao ulitakiwa ukamilike ifikapo Novemba mwaka huu, lakini hakuna chochote kilichoendelea hadi sasa.

Mhandisi Mativila alisisitiza kuwa serikali inapenda kuona makandarasi wazawa wanashiriki kikamilifu katika sekta ya ukandarasi, lakini changamoto imekuwa baadhi yao kutokuwa waaminifu, kuchukua fedha na kushindwa kutekeleza miradi kwa wakati.

Amesema hali hiyo inaleta athari kubwa kwa wananchi, hasa ikizingatiwa mvua kubwa za mwaka 2023 na 2024 ziliharibu makazi na mashamba ya wananchi wa Rufiji, hivyo suluhisho la kudumu ni kuboresha miundombinu ya barabara na mifereji ya maji.

 “Inasikitisha kuona kampuni zenye majina makubwa zinachukua tenda na malipo ya awali, lakini kushindwa kutekeleza majukumu yao. Hatua kali zitachukuliwa, ikiwemo kushikilia vifaa vyao vilivyotelekezwa kwenye maeneo ya miradi na kuzuia wasipewe kazi nyingine kupitia TAMISEMI,” aliongeza.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahimu Kibasa, alisema juhudi mbalimbali zimefanyika kuwasiliana na makandarasi hao kwa njia ya simu, lakini hawapokei. Alifafanua kuwa mradi wa HariCom ulitakiwa kuanza Aprili 10 mwaka jana, huku wa Trinity ukianza Agosti mwaka jana, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea licha ya kupokea fedha za awali.

Katika ziara hiyo, miradi mingine inayoendelea Rufiji ilikaguliwa na wasimamizi wake wameahidi kukamilisha kwa wakati. Pia, wananchi wametakiwa kuhakikisha wanatunza mitaro ya maji iliyojengwa ili itumike kwa kupitisha maji na si kutupa taka. Aidha, halmashauri ya Rufiji imeagizwa kuendelea kutoa elimu ya usafi wa mazingira kwa wananchi wake.