Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, ameanza rasmi kampeni zake mkoani Dar es Salaam ambapo atafanya mikutano kwa siku 10 mfululizo, huku akituma salamu kwa wapinzani wake kwamba tayari upepo wa siasa umebadilika.
Akihutubia leo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mbagala, baada ya kuingia jijini Dar es Salaam akitokea kwenye mikutano ya kampeni iliyofanyika katika mikoa 18 tangu kuzinduliwa kwa kampeni Agosti 31, Mwalimu amesema kuna watu waliomdharau mwanzoni alipoteuliwa, lakini sasa wameanza kuogopa baada ya kusikia sera zake.
“Mwanzoni nilipoanza walinidharau, lakini kwa siku 33 nilizozunguka mikoa mbalimbali nikimwaga sera zangu, wameanza kuogopa. Wanaanza kukaa vikao, mijadala imekuwa mingi – wanaogopa. Natuma salamu kwamba sitapumzika, nitaingia kila mahali kuitafuta kura, sitachoka mpaka kieleweke,” amesema Mwalimu.
Amesema dhamira yake kubwa ya kugombea urais ni kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, hususani kupambana na umasikini wa kipato unaowakabili Watanzania wengi.
Mwalimu ameongeza kuwa nchi zilizoendelea zimepiga hatua kubwa za maendeleo kwa sababu zimeweka mifumo bora ya kusimamia na kutumia rasilimali zake, na kwamba Tanzania pia inaweza kufikia mafanikio makubwa kwa kusimamia rasilimali kwa uwajibikaji na uadilifu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED