Wananchi watakiwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 07:45 PM Oct 03 2025
Wakili Willbard Kilenzi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Wakili Willbard Kilenzi.

Wananchi wameshauriwa kutumia kura zao kama njia sahihi ya kuonesha maoni na kufanya maamuzi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, badala ya kushiriki maandamano ambayo mara nyingi husababisha madhara kwa jamii na taifa.

Wito huo umetolewa leo jijini Mwanza na Wakili Willbard Kilenzi alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari, ambapo alisisitiza kuwa jukumu la kulinda usalama wa nchi si la Serikali pekee au vyombo vya dola peke yao, bali ni wajibu wa kila mwananchi.

Amesema badala ya kufikiria maandamano, wananchi wanapaswa kusikiliza kwa makini kampeni na ilani za vyama vyote, kisha wakajitokeze kupiga kura kwa wingi ili kuunda Serikali itakayowakilisha matakwa ya walio wengi.

“Tumeshuhudia katika baadhi ya nchi jirani jinsi maandamano yalivyopelekea uharibifu wa miundombinu, uporaji, vifo, watoto kubaki yatima na familia kusambaratika. Wenye nia ovu hutumia maandamano kama kisingizio cha kufanya uhalifu,” amesema Kilenzi.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Kilenzi amesema ucheleweshaji au usimamizi usioridhisha wa miradi inayogharimu fedha nyingi za Serikali unaweza kuchochea wananchi kupoteza imani na hata kufikiria maandamano. Hivyo, aliwataka watumishi wa umma na viongozi kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi ili wananchi wapate huduma bora bila malalamiko.

Aidha, ameishauri Serikali kuongeza umakini katika usimamizi wa sheria na kuhakikisha watumishi wasiotekeleza majukumu yao kwa ufanisi wanawajibishwa kinidhamu au kisheria inapobidi, kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.