Dereva ajali iliyoua tisa akiri makosa 64 kortini

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 11:12 AM Oct 31 2024
Dereva wa kampuni ya mabasi ya Ahsante Rabi, Shedrack Swai (37), aliyesababisha ajali iliyopoteza maisha ya watu tisa na majeruhi 54, eneo la Ukiriguru, Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza,  Oktoba 22 mwaka huu, akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi.
Picha: Neema Emmanuel
Dereva wa kampuni ya mabasi ya Ahsante Rabi, Shedrack Swai (37), aliyesababisha ajali iliyopoteza maisha ya watu tisa na majeruhi 54, eneo la Ukiriguru, Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Oktoba 22 mwaka huu, akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi.

DEREVA wa Kampuni ya Mabasi ya Ahsante Rabi, Shedrack Swai (37), anayedaiwa kusababisha ajali iliyoua watu tisa na kujeruhi 54, amekiri makosa 64 katika Mahakama ya Wilaya ya Misungwi.

Dereva huyo alipandishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Esther Marick, na kusomewa shtaka katika kesi ya trafiki namba 30855/2024 inayomkabili.

Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Ramson Salehe, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Lilian Meli, alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo kinyume cha Kifungu cha 41, 63 (2) (b) na 27 (1) cha Sheria ya Usalama Barabarani Namba 168, Marejeo ya Mwaka 2002.

Alidai kuwa Swai alisababisha ajali hiyo Oktoba 22, mwaka huu, eneo la Ukiliguru,  Misungwi, mkoani Mwanza.

Mwendesha mashtaka alidai dereva huyo anakabiliwa na shtaka la kuendesha gari kwa uzembe katika barabara ya umma lenye makosa 64 yakiwamo kuendesha gari kwa uzembe, kusababisha vifo, majeruhi,  uharibifu wa miundombinu na mali.

Alidai kuwa siku ya tukio, mshtakiwa akiwa dereva wa basi lenye namba za usajili T 458 DYD aina ya Yutong, aliendesha kwa uzembe katika barabara ya umma ya Mwanza - Shinyanga katika kijiji cha Ukiriguru.

Alidai kuwa alilipita gari lingine bila kuchukua tahadhari na matokeo yake kuligonga basi lenye namba za usajili T 281 EFG aina ya Yutong na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Baada ya kumsomea shtaka hilo, mshtakiwa alikiri kutenda makosa hayo yote 64 ndipo Wakili wa Serikali Mwandamizi Meli aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Hakimu Marick alimweleza mshtakiwa kuwa shtaka linalomkabili linadhaminika,  hivyo kumtaka kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho kutoka serikali ya mtaa, kitambulisho cha taifa (NIDA) na bondi ya maneno ya Sh. milioni tano kila mmoja. 

Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana baada ya mdhamini mmoja kukosa kitambulisho halisi cha NIDA, hivyo kupelekwa rumande katika Gereza la Butimba,  Mwanza hadi masharti hayo yatakapotimizwa.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 5, mwaka huu, itakapoitwa kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.