Dk. Jafo ajivunia maendeleo sekta ya elimu, afya jimboni kwake

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 03:17 PM Jul 15 2024
MBUNGE wa Kisarawe Dk.Selemani Jafo.
Picha: Julieth Mkireri
MBUNGE wa Kisarawe Dk.Selemani Jafo.

MBUNGE wa Kisarawe Dk.Selemani Jafo amejivunia maendeleo katika Kata ya Msimbu ambapo shule za msingi nyingi zimejengwa kuondoa adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.

Mbali ya shule pia zahanati imejengwa na kuwaondolea usumbufu wananchi kufuata huduma za afya kwa kutembea umbali mrefu.

Dk. Jafo ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara ameyasema hayo alipokuwa katika mkutano na wananchi wa kata ya Msimbu uliofanyika katika eneo la Majumba sita ukilenga  kusikiliza kero za wananchi na kuelezea yaliyofanyika katika eneo hilo na Wilaya ya Kisarawe.

Amesema Serikali inaendelea kuidhinisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe na kwamba kata hiyo ni kati ya wanufaika wa miradi ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati na sasa  barabara ya Homboza ambayo kwasasa ujenzi wake unaendelea.

Pia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kuhakikisha ifikapo Januari 2025 watoto wanaotoka eneo la Kichangani wanasoma ndani ya eneo lao na kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu.

Akizungumzia adha ya barabara ya Homboza Dk Jafo amesema tayari Serikali imeidhinisha sh. milion 200 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo katika awamu ya kwanza.

Mkuu wa Wilaya hiyo Petro Magoti amesema tayari amekubaliana na wamiliki wa malori yanayobeba mchanga kusitisha safari zao katika barabara hiyo kupisha ujenzi Ili ukamilike kwa muda uliopangwa.