Dk.Slaa: CHADEMA haitakufa kwa migogoro

By Enock Charles , Nipashe
Published at 03:31 PM Apr 05 2025
 Dk.Wilbroad Slaa
PICHA: MTANDAO
Dk.Wilbroad Slaa

KADA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk.Wilbroad Slaa amesema si mara ya kwanza kwa chama hicho kupitia misukosuko kutokana na mitazamo tofauti ya wanachama wake na kwamba chama hicho hakiwezi kufa.

Akizungumza katika mjadala katika televisheni moja ya mtandaoni kuhusu mvutano wa kisiasa ulioibuka katika chama hicho kwenye mitandao ya kijamii, ukihusisha makundi mawili yenye mitazamo tofauti kuhusu ushiriki wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Dk Slaa amesema ni mvutano wa kawaida.

Mvutano huo unahusisha kundi la watia nia 55 (maarufu kama G55) waliomwandikia Katibu Mkuu wa chama, John Mnyika, waraka wa wazi wakitoa hoja tisa za kupinga msimamo wa chama wa kutoshiriki uchaguzi bila kufanyika kwa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, msimamo unaojulikana kama “No Reforms, No Election.”

 “Kwa uzoefu wangu chama kina utaratibu wa kuchukua hatua katika kila jambo na si mara ya kwanza kwa jambo kama hili kutokea, sidhani kama ni kitu ambacho kesho asubuhi tu mtu atafukuzwa kwa sabbat ni lazima mchakato ufanyike kwa mujibu wa kanuni za CHADEMA”. amesema Dk.Slaa.

Dk Slaa ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kwa kipindi cha miaka 10 amesema migogoro ya aina hiyo ni ya kawaida na kwamba haiwezi kukiua chama hicho kama ambavyo imeelezwa na baadhi ya wananchi.