Geofrey Kiliba, rais mpya wa TAHLISO

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:32 PM Apr 05 2025
Geofrey Kiliba, mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT),
Picha: Mpigapicha Wetu
Geofrey Kiliba, mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT),

Geofrey Kiliba, mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT), ametangazwa rasmi kuwa Rais mpya wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) kwa mwaka wa uongozi 2025/2026, katika uchaguzi mkuu uliofanyika leo visiwani Zanzibar.

Kiliba alipata ushindi huo mkubwa kwa kuungwa mkono na kura nyingi kutoka kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAHLISO, ambao wanawakilisha serikali za wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu nchini.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Kiliba aliwashukuru wajumbe kwa imani waliyoionesha kwake, na kuahidi kuwa kiongozi mwenye maadili, uwazi, ushirikiano na weledi katika kutekeleza majukumu yake. Aliahidi kujenga TAHLISO imara, yenye kusikiliza na kutetea maslahi ya wanafunzi kwa nguvu na hekima.

“Nitakuwa kiongozi mwenye masikio makubwa na mdomo mdogo; niko tayari kusikiliza hoja na haja zenu. Sote tuna ndoto za kuwa viongozi, lakini leo naomba mtangulize maono ili nitimize ya kwetu sote,” alisema Kiliba kwa unyenyekevu mkubwa.

Wajumbe wengi waliohudhuria mkutano huo walieleza matumaini yao makubwa kwa uongozi mpya, wakisema Kiliba anaonyesha dira, maono na dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko chanya ndani ya jumuiya hiyo ya kitaifa.

Ushindi wa Kiliba unakuja wakati ambapo TAHLISO inategemewa kuwa sauti thabiti ya wanafunzi, hususan katika kushughulikia changamoto zinazowakabili vyuoni na kuhakikisha maslahi yao yanatetea kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.