Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi wakazi wa Jiji la Mbeya kuwa serikali yake itaweka taa za barabarani ili kuruhusu vijana kufanya biashara saa 24 na kukuza uchumi wa mkoa huo.
Dk. Samia ametoa ahadi hiyo leo, Septemba 4, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mbeya Mjini, uliovuta maelfu ya wananchi waliokusanyika kumsikiliza akinadi sera na ilani ya chama chake.
“Mbeya imekua kibiashara, miundombinu imeboreshwa na vijana wanataka kujiajiri. Pamoja na yaliyoahidiwa kwenye ilani, jiji la Mbeya litawekewa taa za barabarani ili vijana wafanye kazi wakati wote. Wizara husika itakuja kuweka,” amesema.
Amebainisha kuwa taa hizo zitafungwa katika maeneo ya Ilomba, Isaye, Meta, njia panda kuelekea Chunya, Rift Valley, Uyole, Kyela na maeneo mbalimbali ya Mbeya Mjini.
Aidha, Dk. Samia amesema endapo atapata ridhaa ya kuiongoza nchi kwa muhula mwingine, serikali inafikiria kujenga daraja la watembea kwa miguu eneo la Mwanjelwa ili kupunguza msongamano na kuongeza usalama wa wananchi.
“Ndani ya Mbeya, baada ya kuhamasisha kilimo na kuleta umeme, kinachofuata ni kuweka kongani za viwanda. Vijana watafanya kazi na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na hata madini,” ameahidi.
Kadhalika, ameahidi serikali kuunga mkono Chama cha Ushirika Kyela katika kuanzisha kiwanda cha kakao, akisema serikali itawekeza nguvu kubwa katika uendelezaji wake.
Awali, mgombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia CCM, Dk. Tulia Ackson, amesema wananchi wa jimbo hilo wamemhakikishia mgombea urais wa chama hicho kura za ushindi na za heshima kutokana na miradi mikubwa iliyotekelezwa.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na sekta ya afya iliyopokea zaidi ya Sh bilioni 200, elimu Sh bilioni 31.1, maji Sh bilioni 30, ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi kwa Sh bilioni 21.7, pamoja na ujenzi wa Soko la Matola uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 6.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED