JWTZ yakanusha taarifa za kuwapo maandamano

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:53 PM Nov 14 2025
Kanali Bernard Mlunga
Picha: Mtandao
Kanali Bernard Mlunga

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekanusha taarifa inayosambaa mitandaoni ikidai kuwepo kwa maandamano, likiielezea kama uzushi unaolenga kuwapotosha wananchi na kusababisha vurugu pamoja na uvunjifu wa amani nchini

Kupitia taarifa yake kwa umma,iliyosomwa  na Kanal Bernard Mlunga imesema JWTZ limewataka watanzania kupuuza tangazo hilo na kuwa waangalifu dhidi ya upotoshaji unaofanywa kupitia mitandao ya kijamii.

Aidha, amesema jeshi hilo limekemea vikali tabia inayozidi kushamiri ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, hasa pale inapolihusisha Jeshi la Wananchi na masuala ya kisiasa kwa nia ya kupotosha na kuzua taharuki miongoni mwa wananchi.

Amesema JWTZ imeeleza  kuwa litaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaojihusisha na vitendo vya upotoshaji kupitia mitandao.