Kwanini Dk. Mwigulu Nchemba?

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:39 PM Nov 13 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu wa Tanzania Dk Mwigulu Nchemba .

UBISHI kuhusu nani atakayekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania umekwisha. Dk Mwigulu Nchemba ameteuliwa na kuidhinishwa na bunge kushika wadhifa huo. Swali limebaki kwanini yeye?

Msingi wa swali hilo, unajengwa na uhalisia kuwa, pengine Dk. Mwigulu alikuwa katika hisia za wachache, ukilinganisha na walivyotabiriwa wanasiasa wengine kuushika wadhifa huo.

Ingawa Mbunge huyo wa Iramba Mashariki hakutarajiwa na wengi kuushika wadhifa huo, wachambuzi wa siasa wanasema ndiye aliyekuwa turufu kwa nafasi hiyo kutokana na uzoefu, historia yake, uwezo na uadilifu wake.

Wachambuzi hao wamekwenda mbali zaidi na kuweka wazi, uteuzi wa Dk. Mwigulu umezingatia mahitaji ya sasa ya kiongozi wa nafasi hiyo, hasa ukizingatia ana umri wa katikati, si kijana sana, wala mzee.

Kwa takriban muongo mmoja, nafasi hiyo imekuwa chini ya Kassim Majaliwa, aliyejulikana kwa utulivu, unyenyekevu na uwezo wa kudhibiti mifumo ya serikali.

Kumrithi mtu wa aina hiyo si jambo dogo. Hata hivyo, uteuzi wa Dk. Mwigulu unaonekana kuwa hatua ya makusudi inayolenga kuunganisha nguvu mbili muhimu, uthabiti wa kisera na uthubutu kiuchumi, kama inavyoelezwa na wachambuzi wa siasa.

Akizungumzia hilo, Mchambuzi wa Siasa, Majjid Said anasema Dk Mwigulu ni zao la mfumo wa ndani wa chama na serikali. Amekuwa akionekana kama kiongozi mwenye msimamo usiotetereka katika hoja, hasa katika masuala ya uchumi, fedha na usimamizi wa rasilimali za umma.

Anasema kitaaluma Dk. Mwigulu ni mchumi na ni miongoni mwa viongozi wachache waliochanganya nadharia na vitendo katika siasa za kisasa.

“Wakati wa utumishi wake kama Waziri wa Fedha, amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali kwa wafadhili,” anasema.

Hoja ya Majjid inathibitishwa na ripoti ya IMF ya mwaka 2024 iliyobainisha kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu za Afrika Mashariki zilizoonyesha uthabiti wa kiuchumi baada ya janga la Uviko-19.

Hali hii, kwa sehemu kubwa, inahusishwa na mageuzi ya kiuchumi yaliyoendeshwa chini ya wizara aliyoongoza Dk Mwigulu.

Majjid anasema kwa lugha nyepesi, uteuzi wake ni ujumbe kwamba uchumi ndio msingi wa kisiasa ya awamu hii.

Mwigulu na zama za uongozi wa kiuchumi

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka dira ya kufungua nchi kiuchumi. Hivyo, uteuzi wa Waziri Mkuu mwenye maono ya kiuchumi ni sehemu ya kuimarisha mnyororo wa uongozi unaoelekeza nguvu kwenye mageuzi ya uzalishaji, biashara na uwekezaji.

Dk. Mwigulu ameonyesha uwezo wa kufikiri kimfumo. Akiwa Waziri wa Fedha, aliwahi kusimamia mpango wa kuunganisha mifumo ya mapato ya TRA, bandari na mamlaka nyingine za ukusanyaji, hatua iliyoongeza ufanisi na uwazi wa mapato ya serikali kama inavyoelezwa na Mwanazuoni wa Uchumi, Dk Josephat Werema.

Kwa upande mwingine, anasema Mwigulu anaelewa siasa za ndani kwa undani. Alipitia changamoto nyingi katika ngazi za chama, kuanzia nafasi za juu ndani ya CCM hadi wizara nyeti.

“Hii inamfanya kuwa kiongozi anayeweza kuvuka vizingiti vya urasimu wa kisiasa na kiutendaji,” anaeleza.

Kiongozi wa kizazi kinachobadilika

Dk. Werema anasema wapo wanaoona uteuzi wa Dk Mwigulu kama ishara ya kizazi kipya cha viongozi kinachoanza kushika hatamu serikalini.

“Ana umri wa miaka 49 kiwango kinachomweka katikati ya vijana na wazee. Anaelewa mienendo ya dunia ya sasa, lakini pia ana heshima kwa misingi ya uongozi wa jadi ya Tanzania,” anasema.

Wakati taifa linaingia kwenye enzi za kidigitali na mapinduzi ya viwanda, anasema Tanzania inahitaji viongozi wanaoweza kuzungumza lugha ya namba, teknolojia na sera kwa wakati mmoja.

“Dk. Mwigulu anaonekana kulijua hili. Mara kadhaa amekuwa akisisitiza kwamba uchumi wa leo siyo wa maneno bali wa takwimu,” anasema Dk. Werema.

Anasisitiza hiyo ni falsafa inayoweza kubadilisha namna Serikali inavyopanga vipaumbele vyake, ikitumia ushahidi na utafiti badala ya mazoea.

Uwezo wa kuunganisha sera za Rais

Mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi, Dk. Lazaro Swai anasema Dk. Mwigulu anajulikana kwa uwezo wake wa kufasiri sera kuu za Serikali katika vitendo.

Katika kipindi ambacho Rais Samia ameweka kipaumbele katika diplomasia ya kiuchumi na ujenzi wa miundombinu, anasema Waziri Mkuu anayeelewa falsafa hiyo ni muhimu.

“Kwa mfano, miradi mikubwa kama reli ya kisasa (SGR), Bwawa la Julius Nyerere, na bomba la mafuta la EACOP inahitaji uratibu wa kiuchumi na kisera unaovuka wizara kadhaa.

Ni pale ambapo uongozi wenye mtazamo wa nadharia na utendaji kama wa Mwigulu unakuwa na maana,” anasema.

Kuunganisha bunge na Serikali

Lakini pamoja na sifa zote hizo, anasema Dk. Mwigulu ana kazi kubwa inayomsubiri. Ndiye anayepaswa kuwa kiungo kati ya Bunge na Serikali.

Anasema itamchukua busara na uthabiti kuhakikisha Serikali inaendelea kufanya kazi kwa amani, bila migongano ya ndani, huku ikiheshimu usimamizi wa wabunge.

Anasema historia inaonyesha kwamba Bunge linaweza kuwa eneo la majaribu kwa mawaziri wakuu wapya. Lakini kwa ufasaha wake wa hoja, ukali wenye busara na nidhamu ya kazi, Mwigulu ana nafasi ya kuibadili changamoto hiyo kuwa jukwaa la kujenga imani ya umma.

Sifa nyingine inayotajwa na Dk. Swai ni uzoefu wa Mwigulu katika utumishi wa serikali. Aliwahi kuwa waziri katika wizara nyingi na muda mrefu.