Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, amesema ni muhimu kuwepo umakini kwenye uwekezaji wa miradi ya miundombinu kwani miradi ambayo haiwezi kutekelezeka inaweza kudhoofisha uwezo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutimiza wajibu wake.
Dk. Mpango ameyasema hayo Julai 10, 2025, wakati akifungua mkutano wa 14 wa Kimataifa wa Watunga Sera wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
Amesema, pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Barani Afrika kutumika kuwekeza katika kuendeleza miundombinu ni vema kuhakikisha michango ya wanachama ambayo imetengwa kama kinga dhidi ya misukosuko ya kiuchumi na kijamii pamoja na kukabiliana na umaskini inabaki kuwa ya kutosha kukidhi malengo ya msingi ya uanzishwaji wake.
Kabla ya kufungua mkutano huo, Dk. Mpango alipata fursa ya kutembelea banda la PSSSF akiwa ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenan Kihongosi, watendaji wa ASSA ambapo walipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Dk. Rhimo Nyansaho.
Lengo la mkutano huo ni pamoja na kuwakutanisha wadau, watunga Sera, wasimamizi na watendaji wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Afrika ili waweze kwa pamoja kujadili na kuazimia namna Sekta hiyo ilivyokuwa na uwezo mkubwa katika ujenzi wa miundombinu na huduma nyingine za kijamii katika Bara la Afrika.
Jumuiya ya (ASSA) inaundwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoka Nchi 15 za Bara la Afrika ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Sudan ya Kusini, Comoro, Cote d'ivoire, Gambia, Sierra Leone, Mali, Namibia na nchi mwenyeji Tanzania. Kaulimbiu ya mkutano huo wa siku mbili ni 'Sekta ya Hifadhi ya Jamii Chachu ya Maendeleo ya Miundombinu kwa ajili ya masuala ya Kiuchumi na Kijamii katika Bara la Afrika'.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED