Mkurugenzi Kibaha aagiza uchongaji barabara kurudiwa kwa ubora zaidi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:37 AM Nov 14 2025
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, ameonesha kutoridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa mradi wa uchongaji barabara katika mitaa ya Machinjioni na Kilimahewa, na kuagiza kazi hiyo ifanywe upya mara moja ili kukidhi viwango vinavyolingana na malengo ya serikali.

Dk. Shemwelekwa alitoa agizo hilo Novemba 13, wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Tangini, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi inayoendelea katika kata mbalimbali za Manispaa ya Kibaha.

Amesema barabara hizo, zinazogharimu Sh milioni 30 kutoka mapato ya ndani ya Manispaa, hazikuchongwa kwa kiwango kinachostahili na hivyo zimeshindwa kutatua changamoto za wananchi kama ambavyo serikali inakusudia.

“Ndugu viongozi, nimekagua mradi huu wa barabara na niseme wazi sijaridhishwa na kazi iliyofanyika. Lengo la serikali ni kutatua kero za wananchi, lakini kwa hali hii sioni kama tatizo limepatiwa suluhisho,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

Ameagiza mtendaji wa kata kuhakikisha barabara hizo zinachongwa upya haraka, akibainisha kuwa atarudi tena kukagua utekelezaji wake ili kuhakikisha maagizo hayo yamezingatiwa.

Aidha, aliwataka wananchi na viongozi wa kata pamoja na mitaa kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo, ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na kuleta tija kwa jamii.

Katika hatua nyingine, Dk. Shemwelekwa ameidhinisha ujenzi wa makaravati mawili katika eneo la Shule ya Msingi Mamlaka na kwenye kivuko cha Kwa Kwembe, ili kupunguza changamoto za mifereji ya maji zinazoathiri wananchi.

Manispaa ya Kibaha imetenga jumla ya Sh milioni 420 kutoka chanzo chake cha mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara za mitaa, ambapo kila kata imepatiwa Sh milioni 30 kutatua changamoto za miundombinu katika maeneo yao.

IMG-20251114-WA0014.jpg 105.83 KB