Mradi wa barabara ya Kwala-SINO TAN wakamilika, ukiunga mkono ajenda ya uchumi wa viwanda

By Miraji Misala , Nipashe
Published at 10:07 AM Nov 14 2025
Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Kibaha, David Kakole
PICHA: MIRAJI MSALA
Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Kibaha, David Kakole

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kibaha umefanikiwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kwala–SINO TAN yenye urefu wa kilomita 3.6 kwa kiwango cha zege, mradi uliogharimu Shilingi bilioni 9.75.

Barabara hiyo muhimu imejengwa kwa awamu mbili katika mwaka wa fedha 2022/2023 na 2023/2024, ikiwa na lengo la kuunganisha Bandari Kavu ya Kwala na Kongani ya Viwanda ya SINO TAN — maeneo ambayo ni kitovu cha shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Pwani.

Akizungumza wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliotembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TARURA Kibaha, Mhandisi wa TARURA Wilaya ya Kibaha, David Kakole, alisema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuboresha miundombinu ya barabara kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara.

Barabara hii ni nyenzo muhimu katika kufungua fursa za kiuchumi. Itapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari Kavu kwenda kwenye viwanda na kurahisisha shughuli za wananchi wanaoishi katika maeneo haya,” alisema Mhandisi Kakole.

Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea ukuaji wa biashara, kuongeza thamani ya ardhi, pamoja na kutoa ajira kwa wananchi kupitia shughuli za usafirishaji na uzalishaji viwandani.

Mradi huo umetekelezwa na Mkandarasi M/S ESTIM Construction Co. Ltd. Kwa mujibu wa Mhandisi Kakole, TARURA itaendelea kusimamia kwa karibu miradi yote ya ujenzi wa barabara ili kuhakikisha inazingatia viwango vilivyowekwa na kutoa thamani halisi ya fedha za umma.

Tumejipanga kuhakikisha barabara zote tunazojenga zinadumu kwa muda mrefu na zinaendelea kutoa manufaa makubwa kwa wananchi. Ndiyo maana tumezingatia ubora wa juu wa zege katika ujenzi huu,” alisisitiza.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi wa eneo la Kwala, Gerald Thilia, alisema ujenzi wa barabara hiyo umekuwa neema kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuwa umeboresha kwa kiasi kikubwa shughuli za usafirishaji wa mizigo na uwekezaji.

Zamani tulikuwa tunatumia muda mrefu na gharama kubwa kusafirisha mizigo kwa sababu barabara ilikuwa mbovu. Sasa hali imebadilika, magari yanafika kwa urahisi, gharama za usafiri zimepungua na maeneo ya uwekezaji yamekuwa rafiki zaidi,” alisema Thilia.

Barabara hiyo inatarajiwa kuwa chachu ya kuimarika kwa uchumi wa Mkoa wa Pwani, hasa kutokana na nafasi yake muhimu katika kusaidia usafirishaji wa bidhaa na malighafi kati ya Bandari Kavu ya Kwala na viwanda vinavyoendelea kujengwa katika eneo la SINO TAN.