Msiogope, kuna amani na utulivu kuelekea siku ya uchaguzi- RC Malisa

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 05:39 PM Oct 24 2025
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amewataka wananchi mkoani humo kujitokeza kwenye vituo vya kupigia Kura siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu ili watimize haki yao ya kikatiba huku akiwahakikishia kuwa vyombo vya ulinzi na Usalama vimejipanga kuhakikisha hawabugudhiwi.

Malisa ameyasema hayo leo alipozungumza na wandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Uchaguzi huo ambapo amesema wamejipanga kuhakikisha Uchaguzi huo unafanyika kwa amani na utulivu.

Amesema wanasikia na kuona baadhi ya watu wakihamasishana kufanya maandamano siku ya Uchaguzi huo na hivyo amewaonya watu hao kuwa watakumbana na mkono wa Sheria.

"Tunashukuru tangu Kampeni zimeanza mpaka Leo halijatokea tatizo lolote na tutahakikisha utulivu huu unaendelea kulindwa wakati wote, wale wanaojupanga kufanya fujo siku ya Uchaguzi ni vema wakajionya kwanza wenyewe kabla ya kufanya hivyo," amesema Malisa.

Amewashauri wananchi kwenda kuwachagua viongozi ambao wanawaamini kuwa watawaletea maendeleo wanayoyahitaji na kwa kuzingatia sera ambazo walikuwa wanajinadi kwenye Kampeni.