Nyalandu: Vijana jitokezeni kwa wingi kupiga kura Oktoba 29

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 04:59 PM Oct 24 2025
Waziri Mstaafu, Lazaro Nyalandu.

Vijana nchini wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, kama njia ya kutimiza wajibu wao wa kikatiba.

Rai hiyo imetolewa leo na Waziri Mstaafu, Lazaro Nyalandu, wakati wa mahojiano maalum na waandishi wa habari mkoani Mwanza.

Nyalandu amewataka vijana kutumia fursa ya demokrasia na uhuru wa Tanzania kwa kujitokeza kupiga kura, sambamba na kuwasaidia wazee watakapokuwa kwenye foleni za vituo vya kupigia kura.

 “Nawaomba vijana kushawishiana kwenda kupiga kura, kwa sababu vijana wanaposhiriki katika mchakato huu ni jambo jema sana kwa taifa letu. Pia nawaomba mjitahidi kutunza amani, kwani amani ikipotea hairudi kirahisi. Amani ni tunu kubwa sana tuilinde,” amesema Nyalandu.

Ameongeza kuwa jamii inapaswa kuhakikisha hakuna mtu anayeivunja amani iliyopo nchini, huku akitoa wito maalum kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa kujitokeza kwa wingi vituoni siku ya kupiga kura ili kutumia haki yao ya kidemokrasia ipasavyo.