WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, amefanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya rufani ya Mkoa wa Dodoma na kupiga marufuku wanawake wajawazito kusubirishwa mapokezi wakiwa na uchungu wa kujifungua.
Ziara hiyo inakuja ikiwa ni siku moja tangu Dk.Nchemba aapishwe kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan, juzi Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Katika ziara hiyo Dk.Nchemba alipata fursa ya kuzungumza na watumishi, wagonjwa pamoja na ndugu na jamaa wa wagonjwa walifika hospitalini hapo.
Akizungumza na wagonjwa, amewahoji namna ambavyo wamekuwa wakipatiwa huduma za matibabu na watumishi walipo katika hospitali hiyo.
Mara baada ya kumaliza kukagua utoaji huduma katika hospitali hiyo, ametoa maagizo kadhaa kwa hospitali zote nchini ikiwamo kuacha tabia ya kuwasubirisha mapokezi wajawazito wenye uchungu wa kutaka kujifungua.
“Maagizo yangu ni kwamba na hii ni kwa ajili ya hospitali zote nchini kuwa ni marufuku wajawazito kusubirishwa mapokezi kwa ajili ya kuandikishwa bali wapate huduma kwanza na anayehitaji kuwaandikisha awafute huko wodini,” amesema.
Pia, amesema wakati akizungumza na wagonjwa kwenye hospitali hiyo amebaini ipo changamoto ya wajawazito kutohudumiwa kwa kukosa ndoo ama beseni.
“Hospitali inapaswa kuwa na ndoo na beseni za ziada kwa ajili ya kusaidia hawa ambao hawana vifaa hivyo wakati huu ambapo serikali inaendelea kushughulikia suala la bima ya afya kwa wote,” amesema Dk. Nchemba.
Aidha, ameziagiza hospitali zote nchini Wizara ya Afya pamoja na Bohari ya Dawa nchini (MSD), kuweka vipaumbele vya kununua dawa kutokana na mahitaji ya eneo husika.
Amesema, hivi sasa kumekuwepo na tabia hospitali za serikali kutumika kwa ajili ya kutoa vipimo, lakini inapofika suala la dawa wagonjwa wanaambiwa wakanunue maduka ya nje.
“Kama hospitali ya serikali inakosa dawa duka la nje linapataje dawa? hiyo ni tabia ya baadhi ya wataalam kuagiza Panado kwenye hospitali za umma wakijua watawaambia wagojwa wapi pa kuipata dawa hiyo muhimu kwenye vioski vya nje," amesema.
Hata hivyo, amesema, Rais Samia ametumia kiasi kikubwa cha fedha kwenye vifaa tiba na dawa, na kwamba haiwezekani hospitali ya umma ikakosa dawa wakati maduka binafsi zinakuwepo.
Vile vile, ameeleza kuridhishwa na namana hospitli hiyo imekuwa ikitoa huduma kwa wananchi na kuagiza changamoto zilizopo kufanyiwa kazi.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Ibenzi Ernest amemshukuru Waziri Mkuu kwa kuchagua kituo chao na kufanya ziara ya kukagua utoaji huduma za matibabu kwa wananchi.
“Tunamshukuru sana Waziri Mkuu kwa kufanya ziara hii sisi kama watumishi imetupa hamasa ya kufanya kazi kwa ufanisi kuwahudumia wananchi na kuyafanyia kazi yote ambayo ameyaagiza,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED