RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali ya Jamhuri na Zanzibar zitaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya kibiashara na uwekezaji.
Rais Mwinyi amesema hayo jana wakati akizindua rasmi maonesho ya 49 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayofanyika katika viwanja vya sabasaba.
Rais Mwinyi amesema serikali hizo zitaendelea kuwa bega kwa bega katika kushirikiana na wafanyabiashara na wawekezaji.
Amewataka watanzania kuthamini bidhaa za ndani ili kuimarisha soko lake ndani na Kimataifa.
Ameagiza mamlaka za biashara kuhakikisha alama ya biashara na huduma ya Tanzania (Made in Tanzania), inatumika na wafanyabiashara ili itumike kutangaza bidhaa za Tanzania.
Amesema mpango wa serikali ni kuhakikisha inarahisisha mazingira ya biashara na kuimarisha mifumo ya kidijitali katika sekta hiyo.
Rais Mwinyi amepongeza hatua iliyofikiwa na Tantrade ya kuboresha miundombinu katika viwanja hivyo vya maonyesho ya biashara huku akisisitiza kwamba hilo litasaidia kuuweka katika viwango vya kimataifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Latifa Khamis, amesema maonesho ya mwaka huu, wametumia mfumo wa kidijigali kuyaendesha kunzia hatua za awali za kujisajili mpaka sasa.
Pia, amesema mpaka jana Wizara ya Maliasili na Utalii, ndiyo ilikuwa imeongoza kwa watembelaji wengi kwenye maonesho hayo.
Latifa amesema waliotembelea banda hilo la Maliasili na Utalii ni zaidi ya 190,000 kati ya hao watoto ni 54, 000.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED