Tanzania kuendeleza mashirikiano na Ujerumani, UNICEF

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:51 PM Jul 09 2025
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amekutana na kufanya mazungumzo na Elke Wisch, Mwakilishi Mkazi wa UNICEF nchini Tanzania.

Katika mazungumzo yao viongozi hawa wameonesha umuhimu wa maji kwa jamii, afya, elimu na hasa wanawake na watoto. 

Vilevile, Aweso amelishukuru Shirika la UNICEF kwa kuwa mdau muhimu katika miradi ya maji na usafi wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi. 

Tanzania kupitia Waziri wa Maji Aweso amelihakikishia Shirika la UNICEF ushirikiano na ushirikiano na ameliaka kuendeleza ushirikiano.  Kikao hicho pia kumehudhuriwa na Bibi Gemma Querol, Mkurugenzi wa masuala ya maji wa UNICEF.

Katika hatua nyingine kwenye ratiba ya tukio lingine Aweso amekutana na Naibu Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mr Manuel Muller na uongozi wa KFW kwa lengo la kujadiliana masuala ya mashirikiano katika utekelezaji wa miradi ya Maji nchini. 

Katika mazungumzo hayo, Naibu Balozi  wa Ujerumani amefurahishwa na mashirikiano ya muda mrefu baina ya nchi hizi mbili na kueleza kuwa, utekelezaji wa Miradi iliyokamilika imeleta tija kubwa kwa wananchi na ni matarajio hayo hayo yatapatikana kwenye utekelezaji wa Miradi  inayoendelea. 

Aidha, kwa upande wa Serikali, Waziri Aweso ameahidi kudumisha mashirikiano hayo pamoja na kumhakikishia kuwa Miradi inayotekelezwa kupitia mashirikiano haya, itatekelezwa na kukamilika kwa muda uliopangwa. 

Sambamba na hilo, ameeleza kuwa fursa bado ziko nyingi hivyo wanakaribishwa kuendelea kusaidia ili kufikia malengo ya kitaifa ya kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95 mijini ya upatikanaji wa huduma ya maji.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alifafanua kuwa miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo ni sehemu ya awamu ya pili ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji. 

Amesema utekelezaji utafanyika kwa kuzingatia vigezo maalum, huku mamlaka za maji zikipewa jukumu la kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.