Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Pwani umetangaza mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi, matengenezo na ukarabati wa barabara, baada ya kutumia zaidi ya Sh bilioni 53 katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika halmashauri zote tisa za mkoa huo.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Mhandisi Ibrahim Kibasa, akizungumza na waandishi wa habari, alishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za maendeleo ambazo zimewezesha kupunguza changamoto za usafiri na kuongeza ufanisi katika sekta ya barabara.
Fedha tulizopokea zimewezesha kuboresha barabara zinazounganisha maeneo ya uzalishaji, huduma za kijamii, makazi ya watu pamoja na barabara zinazohudumia viwanda,” alisema Kibasa.
Mtandao wa Barabara Mkoa wa Pwani
Akifafanua kuhusu hali ya barabara, Kibasa alisema mkoa wa Pwani una jumla ya km 5,186.053, ambapo:
Km 122.41 ni za lami
Km 894.8 ni za changarawe
Km 4,169.19 ni za udongo
Alisema ukubwa huo wa mtandao unahitaji uwekezaji mkubwa ili kuhakikisha barabara zinastahimili uzito wa magari na wingi wa usafirishaji hasa kwenye maeneo ya uzalishaji.
Fedha Zaidi ya Sh Bilioni 53 Zilizopokelewa
TARURA Pwani ilipokea jumla ya Sh 53,033,278,837.44 kutoka vyanzo mbalimbali vya serikali na washirika wa maendeleo, zikiwemo:
Mfuko wa Barabara (Matengenezo): Sh 6.9 bilioni
Mfuko wa Barabara (Maendeleo): Sh 3 bilioni
Mfuko Mkuu wa Serikali – Majimbo: Sh 4.225 bilioni
Tozo ya Sh 100 kwa lita ya mafuta: Sh 13.875 bilioni
Fedha za Dharura: Sh 7.133 bilioni
Benki ya Dunia (CERC): Sh 17.895 bilioni
Fedha hizi zimewezesha kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imeleta nafuu kwa wananchi na kuboresha usafiri katika maeneo ya kilimo, biashara na viwanda,” alisisitiza Kibasa.
Miradi Iliyotekelezwa na Inayoendelea
Kwa mujibu wa Meneja huyo, miradi imeendelea kutekelezwa katika wilaya zote za mkoa, ikihusisha ujenzi wa madaraja, kalavati, mifereji ya maji ya mvua na matengenezo ya barabara zilizokuwa zikisababisha adha kwa wananchi.
Kibaha Vijijini
Ujenzi wa boksi kalavati Kwala–Mperamumbi
Matengenezo ya barabara ya Picha ya Ndege–Bokotimiza
Matengenezo ya barabara ya Kongowe–Forest Yombo
Rufiji
Ujenzi wa daraja la Mohoro
Ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua Ikwiriri Stand
Matengenezo ya barabara za Ikwiriri mjini
Ukarabati wa barabara ya Utete–Kingupira
Kibiti
Ukarabati wa barabara ya Muyuyu–Ruaruke
Bagamoyo
Uwekaji wa taa za barabarani kwa kuongeza usalama
Chalinze
Ujenzi wa kalavati barabara ya Ruvu–Milo
Miradi mingine inaendelea katika Mkuranga, Mafia na Kisarawe, maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na uharibifu wa barabara kutokana na mvua na shughuli za usafirishaji wa mazao na bidhaa.
Ongezeko la Viwanda Laongeza Mahitaji ya Barabara
Kibasa alisema kuwa hadi kufikia mwaka 2025, Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1,631, vikiwemo:
Viwanda vikubwa: 156
Viwanda vya kati: 190
Vidogo: 268
Vidogo sana: 1,017
Uzalishaji wa viwanda hivyo umefikia zaidi ya tani 194,554,512 kwa mwaka, hali inayoongeza mahitaji ya barabara imara kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa.
Maeneo mengi ya viwanda bado yanategemea barabara za udongo, na hadi sasa barabara za lami zimefikia km 12 pekee,” alieleza Kibasa.
Ahadi ya Kuendelea Kuboresha Miundombinu
Kibasa alisisitiza kuwa TARURA itaendelea kusimamia miradi yote kwa ubora na kasi ili kuhakikisha mkoa wa Pwani unakuwa na barabara za kisasa zitakazowezesha uchumi kukua kwa kasi zaidi.
Tumejipanga kuhakikisha barabara za Pwani zinakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya usafiri na uchumi wa kisasa. Miundombinu bora ndiyo msingi wa maendeleo ya wananchi na wawekezaji,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED