TMA: Kesho ni kupatwa kwa jua, mwezi

By Restuta James , Nipashe
Published at 05:48 PM Sep 06 2025
news
Picha Mtandao
Kupatwa kwa Jua

TANZANIA ni miongoni mwa nchi zitakazoshuhudia tukio la kupatwa kwa jua, litakalodumu kwa takribani saa sita, jioni linapozama hadi saa 5:55 usiku wa kesho Septemba 7, 2025.

Taarifa iliyotolewa leo Septemba 6, na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema kuwa tukio hilo litatokea kwa awamu tatu kuanzia kesho jioni hadi saa 5:55 usiku.

Taarifa hiyo imesema awamu ya kwanza ni kuanzia jioni jua linapozama hadi saa 2:29 usiku, saa 2:30 hadi saa 3:52 usiku na saa 3:53 hadi saa 5:55 usiku, na kwamba litahusisha kupatwa kwa sehemu na kikamilifu.

“Hali ya anga inatarajiwa kuwa yenye mawingu kiasi na kutoa fursa nzuri ya kuonekana kwa tukio hilo kwa macho. TMA inaendelea kufuatilia tukio hili la kupatwa kwa mwezi na itatoa mrejesho kila inapobidi,” imesema.

Imesema tukio la kupatwa kwa mwezi linatokea wakati dunia inapita kati ya jua na mwezi na kusababisha kivuli cha dunia kuwa katika uso wa mwezi, pindi dunia, mwezi na jua, vinapokaa kwenye mstari mnyoofu.

1
Imefafanua kuwa tukio la kupatwa kwa mwezi linaweza kutokea kikamilifu (Umbra), wakati ambao dunia inakuwa imefunika mwanga wote wa jua na kupelekea kivuli kizito (giza), katika uso wa mwezi au kwa sehemu (Penumbra) ambapo Dunia husababisha kivuli hafifu katika uso wa mwezi.

“Tukio la kupatwa kwa mwezi kwa Septemba 07, 2025 (kesho), ni la kupatwa kwa mwezi sehemu na kikamilifu. Tukio hili linatarajiwa kuonekana katika maeneo ya bara la Ulaya, Asia, Australia na Afrika.

“Kwa hapa nchini, hali ya kupatwa kwa mwezi inatarajiwa kuanza kwa kupatwa kwa mwezi sehemu kuanzia pale jua linapozama hadi saa 2:29 usiku na kufuatiwa na kupatwa kwa mwezi kikamilifu kuanzia saa 2:30 hadi saa 3:52 usiku.

“Aidha, tukio hili linatarajiwa kuhitimishwa kwa kupatwa kwa mwezi sehemu kuanzia saa 3:53 hadi 5:55 usiku. Kwa ujumla hali hii inatarajiwa kudumu kwa muda wa takriban saa sita,” imefafanua taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa kwa kawaida, mzunguko wa mwezi una uhusiano mkubwa na kupwa na kujaa kwa maji baharini.

“Hali hii inatarajiwa kuongezeka kwa kina cha maji katika bahari wakati wa tukio hilo. Hata hivyo, hali hiyo haitarajiwi kupekelea athari kubwa,” imesema.