Mradi wa Uendelezaji wa Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) unatekeleza miradi yenye thamani ya Shilingi bilioni 51 katika Jiji la Arusha ikiwa ni sehemu ya uendelezaji wa Jiji hilo katika eneo la miundombinu ya barabara, masoko na stendi.
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Arusha, Mhandisi Godfrey Bwire wakati akitoa taarifa ya hali ya utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na TACTIC katika Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwa ni miongoni mwa Majiji yanayonufaika na mradi huo.
Amesema mradi wa TACTIC katika Jiji la Arusha unatekeleza ujenzi wa barabara zenye urefu wa Km 10.2 ambazo ni pamoja na barabara ya Oljoro Km 1.45, barabara ya Olasiti Km 3.96 na barabara ya Ngoselotoni Km 4.8 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 72 na inagharimu shilingi bilioni 20.7
Vile vile, Mhandisi Bwire amesema kuwa mradi huo unatekeleza miradi mingine ya ujenzi wa Soko la Kilombero, ujenzi wa stendi mpya ya kisasa ya Bondeni City kwa ajili ya mabasi ya mikoani ambayo inajengwa katika kata ya Murieti pamoja na kuboresha eneo la kuuzia nyama choma la Kwa Mromboo ambapo litajengwa soko jipya katika eneo hilo na kuongeza kuwa ujenzi wa miradi hiyo umefikia asilimia 6 na inagharimu shilingi bilioni 30.6.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk. Maduhu Nindwa amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha wameipokea kwa furaha kubwa miradi hiyo kwa sababu wameiona faida kubwa kabla hazijatokea kwa mtu mmoja mmoja mpaka ngazi ya mkoa na taifa pia.
"Tulipokea miradi hii kwa upekee na kwa heshima kubwa kwa Serikali yetu kutukumbuka kwamba tuna uhitaji wa hii miundombinu ambayo itasaidia moja kwa moja kukuza biashara hususani katika ujenzi wa masoko ya Kilombero, soko la kwa Mromboo na ile barabara ya kwenda mji wa Bondeni City", amefafanua.
Dk. Nindwa amebainisha kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara itasaidia pia katika maeneo mengine ya utoaji huduma za kijamii hasa elimu na afya.
Amesema kwa upande wa elimu kutakuwa na magari mengi ya abiria ambayo yatapita katika barabara hizo kwa hiyo wanafunzi watachukuliwa kwa urahisi na kufika shuleni kwa wakati hivyo kusaidia kupandisha kiwango cha elimu katika Jiji hilo.
"Kwa upande wa afya, tunafahamu kwamba Mhe. Rais alianzisha mfumo wa usafirishaji wa akina mama na watoto kwa njia ya dharura kwa kutumia ambulance za jamii maarufu kama 'm-mama', ujenzi wa barabara hizi utasaidia watu wengi kuwachukua akina mama wenye changamoto kutoka kwenye mitaa yetu na kuwawahisha hospitali kupata huduma kwa hiyo moja kwa moja unaona miradi hii inalenga kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga", amebainisha.
Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Oloresho, James Stephano amesema ujenzi wa barabara ya Oljoro utasaidia kurejesha biashara pembezoni mwa barabara hiyo zilizokuwa zimefungwa kutokana na kukosekana kwa wateja walioacha kutumia barabara hiyo kwa sababu ya ubovu wa barabara hiyo, lakini baada ya barabara hiyo kujengwa biashara zimerejea tena katika mtaa wake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED