Mwenyekiti wa Mamalishe awataka wajasiriamali Singida kumsapoti Samia

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 12:16 PM Sep 08 2025

Mwenyekiti wa Mamalishe Tanzania, Havijawa Omary.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Mamalishe Tanzania, Havijawa Omary.

Mwenyekiti wa Mamalishe Tanzania, Havijawa Omary, amewaomba viongozi wa wajasiriamali wa Mkoa wa Singida kumsemea vizuri Rais Samia Suluhu Hassan, mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili ashinde kwa kishindo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza jana katika kongamano la wafanyabiashara wadogo mkoani humo lililofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na machinga, bodaboda, mama na baba lishe, wavuvi, wasusi na mafundi ujenzi, Omary alisema Rais Samia amefanya mambo makubwa kwa ajili ya wajasiriamali, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kumuunga mkono.

“Napiga magoti hapa, nyie wote ni viongozi, ninawaomba mkamsemee mama Samia mazuri ili aweze kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huu. Rais amefanya mambo makubwa na ya msingi, ndiyo maana tupo kila mkoa kushiriki kwenye makongamano kuhakikisha tunayasema mazuri aliyoyafanya, hasa kwenye kundi letu sisi wajasiriamali bila kumsahau mama lishe,” alisema Omary.

Alibainisha kuwa mamalishe na wajasiriamali wengine wamekuwa miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mikopo inayotolewa na serikali kupitia asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri za Wilaya kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

“Hatuwezi kuwahamasisha mama lishe watumie nishati safi bila kuona mafanikio. Mamalishe ni wanufaika wa kwanza wa mikopo hii, na mimi nikiwa Mwenyekiti wa Taifa pia ni mnufaika wa mikopo inayotolewa na Rais kupitia mfumo huu,” alisema.

Omary alisema Rais Samia alishatenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali wadogo lengo likiwa kuboresha biashara zao na kujikwamua na umaskini.

Alifafanua kuwa huko nyuma mamalishe walikuwa wananyimwa mikopo kutokana na mazingira magumu ya biashara zao, lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani wameanza kupata mikopo kuanzia shilingi 100,000 hadi milioni 4.

“Tulikuwa tunanyimwa mikopo sisi mamalishe, lakini sasa mambo ni mazuri. Kwanini tusisimame kusema mazuri aliyoyafanya Rais, hasa kwenye kundi letu?” alisema.

Omary pia aliwasihi wajasiriamali wadogo kujitokeza kwa wingi kuchukua vitambulisho vya ujasiriamali ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.

Aidha, aliishukuru Idara ya Maendeleo ya Jamii chini ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, kwa kazi nzuri anayofanya ambayo imesaidia kuinua heshima ya wajasiriamali nchini.